Wazazi watakiwa kutowapa watoto Simu


Na Ferdinand Shayo, Arusha

Serikali Mkoani Kilimanjaro imewataka wazazi na walezi wa watoto kutowapa watoto wao simu za mkononi wanapokwenda shuleni kwa kuwa zinawaingiza katika matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, kuhatarisha maisha yao, wasichana kupata mimba za utotoni na hivyo kupoteza ndoto zao za maisha bora.


Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dr. Anna Mghwira, Bw. Flugence Mponji ametoa changamoto hiyo wakati alipozungumza na wazazi, walezi na waalimu  wa shule ya sekondari ya Elimo katika siku maalum ya wazazi ambayo hutumiwa wazazi kuja kuwasalimia watoto wao  shuleni.

Bw. Flugence Mponji amesema, mitandao ya kijamii imekuwa ikiwapotosha vijana hasa wanafunzi wa shule za sekondari ambao wanaiga tamaduni za kigeni na hata kusababisha majanga kama ilivyotokea wilaya ya chunya ambako wanafunzi wanatuhumiwa kuhusika na  moto ulioteketeza mabweni mawili ya shule ya  sekondari ya kiwanja kutokana na matumizi ya simu.

Ameagiza kufanyika ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mabweni ya wasichana na wavulana ili kujiridhisha kama wanafunaazi hawakai na simu kwenye mabegi yao kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya simu.

Mkuu wa shule hiyo Bw. Elisamehe Kimaro amesema, ingawa wanakabiliwa na changamoto la bwalo la chakula lakini mwaka ujao wataanzisha madarasa ya kidato cha tano na sita na  madarasa ya elimu ya awali ambayo majengo yake yamekamilika kwa hatua zote.