CCM Njombe watangaza kupita bila kupingwa



Na Amiri kilagalilil-Njombe

Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kimewatangazia wananchi kutokuwa na uchaguzi wa viongozi serikali za mitaa katika mkoa huo unaotarajia kufanyika siku ya kesho Novemba 24 kwa kuwa kimepita bila kupingwa katika vijiji, mitaa na kata zote katika mkoa huo,hivyo wananchi waweze kuendelea na shughuli zao.

Akizungumza na vyombo vya habari  katika ofisi za chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe katibu  wa siasa na uenezi wa chama hicho mkoa Erasto Ngole, amesema siku ya kesho hakutakuwa na kazi ya kupiga kura hivyo wananchi na wanachama wa chama hicho kuendelea na kazi nyingine.

“Kesho ni siku ya uchaguzi zipo fununu mtaani kwamba wenzetu Chadema wanajiandaa kuandamana siku ya kesho,kwasababu sisi ni chama cha mapinduzi nilitaka kuwaambia wananchi na wana CCM wenzangu,kwa kuwa kesho hatuna kazi ya kupiga kura niwatake wanaNjombe na wana CCM tukaendelee kazi zingine”amesema Ngole.

Ngole ameongeza kuwa wananchi wasipotoshwe na mwanasiasa yeyote kwa kuwa mara baada ya kuapishwa viongozi hao watakuwa ni viongozi wa serikali hivyo atakayesema hamtambui watakutana na taratibu za kisheria.

Wakati hayo yakijiri mkoani Njombe kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hapo kesho, waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa, Selemani Jafo, amewataka wananchi kushiriki katika zoezi hilo bila kujihusha na viashiria vya uvunjifu wa amani au kuvuruga uchaguzi huo.

Pia amesema uchaguzi huo utafanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini isipokuwa mikoa mitatu ya Katavi, Ruvuma na Tanga ambapo wagombea wake katika vyama mbalimbali walipita bila kupingwa.