China yasema inaendeleza mazungumzo na Marekani

Afisa wa wizara ya fedha ya China amesema nchi yake inaendelea na juhudi za kutatua mgogoro wa kibiashara na Marekani, akitupilia mbali shutuma kwamba mazungumzo hayo yamekwama na kuzieleza kuwa ni za uzushi.

Msemaji wa wizara hiyo, Gao Feng amesema leo kwamba hawezi kudhihirisha taarifa zaidi, lakini China itaendelea kutafuta makubaliano na Marekani. "China iko tayari kufanya kazi na Merekani kwa misingi wa usawa na kuheshimiana, kushughulikia vizuri maswala ya msingi ya kila mmoja na kujitahidi kufikia makubaliano ya awamu ya kwanza.

Hii ni kwa sababu ya maslahi ya China na Marekani. Na vile vile maslahi ya ulimwengu," amesema Gao.

Maafisa kutoka pande zote mbili wamesema, masoko ya biashara yamekuwa yakipanda na kuporomoka kulingana na ripoti za mgogoro huo.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kabla ya mwezi huu kumalizika anatarajia kusaini makubaliano ya awali na kiongozi wa China Xi Jinping.