Jinsi ya kuishi na mtu mwenye wivu katika mahusiano ya kimapenzi


Mtu mwenye mafanikio kwenye mapenzi ni yule anayeamini katika saikolojia ya kujitambua. Hapa nikupe msisitizo kuwa ni lazima ujitambue ili uweze kuwa bora kwenye mapenzi. Kama hujitambui, maana yake hutajua ulitendalo.

Ikiwa utashindwa kujua ulitendalo, wewe utageuka kuwa kero kwa mwenzi wako. Ukifikia hatua hiyo, unadhani ni nani anaweza kukuelewa? Ni vema ujijue, ujifahamu kasoro na uimara wako katika uhusiano wako. Kama unamfurahisha au kumchukiza, yote yanafaa kugota ndani ya kichwa chako.

Je, una wivu? Hilo unapaswa kulitambua kwa sababu lipo ndani yako. Bahati mbaya ni kwamba watu wanakuwa na wivu wa kupitiliza lakini wakiambiwa wanakuwa wakali. Wanadai wanasingiziwa.

Ni vizuri ukatambua upungufu ulionao kabla ya kuelezwa na mtu wa pili.

Wivu wako umekugharimu mara ngapi? Makala haya yanatosha kuwa tiba yako ya kudumu. Pengine hujawahi kukaa, ukatafakari na kugundua kuwa wivu wako unakupeleka njia isiyo sahihi kimapenzi, hapa chini kuna mambo  ambayo ni muongozo madhubuti.

Jifunze kwa watu wengine.
Mara nyingine ni rahisi kugundua kuwa unafanya makosa baada ya kuwaona wengine na kujifunza kutoka kwao. Hivyo basi, jaribu kuwaangalia watu wengine walio kwenye uhusiano. Fuatilia mtindo wao wa maisha, mafanikio yao kisha ujitazame wewe.

Bila shaka hapo ulipo, utakuwa umeshawahi kujionea wanaume na wanawake wenye wivu, jinsi wanavyotenda mambo yao, wanavyoudhi na kuchukiza kwenye uhusiano. Kama ndivyo, basi hilo ni somo kwako kwa kuepuka yale yaliyowafanya wachukize.

Inawezekana ukawa umeona kupitia kwa macho yako au umesimuliwa. Muhimu kutambua ni kwamba hulka za wivu, hususani unapozionesha mbele za watu wa pembeni ni mbaya. Kwa mantiki hiyo, kama utaweza kutambua na kuelewa alama za wivu, sina shaka kuwa utakuwa unaweza kujua jinsi ya kuishi katika mazingira salama.

Mpe nafasi
Kumbana mwenzi wako haina maana ndiyo utamfanya adumishe uaminifu kati yenu. Jifanye kama mtu usiyejali, muache atoke na marafiki zake. Inaweza kuwa tatizo endapo ataona unamnyima uhuru anaoutaka. Anahitaji nafasi ya kufurahi na marafiki zake, unambana kwa nini?

Akilini kwako lazima ukubali kwamba mwenzi wako ni mtu mzima na anajitambua, kwa hiyo uhuru utakaompa, utawezesha yeye kujiamini zaidi na kuheshimu uaminifu wako kwake. Kisaikolojia, mwenzi wako akigundua unamuamini, naye huzidisha upendo.

Vizuri pia kutambua kuwa wivu hukua zaidi pale mmoja anapokuwa na hisia kwamba mwenzi wake anasaliti. Kama upo kwenye uhusiano wenye afya, huhitaji kusumbuliwa na mawazo mabaya. Endapo utashindwa kuondoa wingu la shaka ndani yako, kaa ukijua kuwa unajiharibia.

Ongeza uaminifu.
Mojawapo ya dawa nzuri ya kukabiliana na wivu ni kuongeza kiwango cha uaminifu. Muamini mwenzi wako na utaona jinsi mambo yatakavyokwenda. Tunza akilini kwamba kutengeneza uhusiano imara na wenye mafanikio, huhitaji kiwango kikubwa cha uaminifu.

Amini kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo. Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda ‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.

Kwa kawaida, anaweza kuwepo mtu ambaye atakufanya usimuamini mwenzi wako hata kidogo. Inawezekana akakujengea picha kutokana na maneno ya zamani au matukio yaliyopita. Je, unaona wivu kwa sababu umeambiwa mpenzi wako aliwahi kutoka na watu wawili tofauti kabla yako?

Wivu wa nini? Kwa nini maneno hayo yakuchanganye akili? Je, ulimkuta akiwa mbumbumbu wa mapenzi na hajawahi kutoka na yeyote? Kumbe utabaini kuwa historia ya mwenzi wako haina maana inayokubalika kwenye uhusiano endelevu.

Wanasema shetani wa jana, leo anaweza kuwa malaika. Vilevile malaika wa leo kesho anaweza kuwa shetani. Inawezekana hao ulioambiwa alitoka nao walimtenda ndiyo maana hakuwapa nafasi ya kudumu lakini wewe umepata fursa hiyo kwa sababu unakidhi mahitaji yake.