Mbunge wa CCM ataka uzazi wa mpango kwa wanaume


Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Khadija Nassir, ameitaka serikali kuanzisha programu za uzazi wa mpango kwa wanaume kwa kuwa utafiti mbalimbali unaonyesha wana uwezo wa kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni, Mbunge huyo alisema utafiti mbalimbali duniani unaonesha kwamba mwanaume mmoja ana uwezo wa kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja, wakati mwanamke mmoja ana uwezo wa kushika mimba moja kwa miezi tisa.

“Je, serikali haioni sasa kuendelea na program za uzazi wa mpango ni uharibifu wa rasilimali badala yake programu za uzazi wa mpango zifanyike kwa akina baba?”alihoji.

Akijibu, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Faustine Ndugulile, alisema ni dhana potofu kwamba uzazi wa mpango ni wanawake peke yao.

“Suala la uzazi wa mpango linawahusu wanaume vile vile na sisi kama serikali tunahamasisha kinababa na mama kushiriki kwenye uzazi wa mpango salama,” alisema.