https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mikoa Mitatu haifanyi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa | Muungwana BLOG

Mikoa Mitatu haifanyi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa


Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza kuwa mikoa mitatu haitafanya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa wagombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepita bila kupingwa.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mwita Waitara amesema hapo jana jijini Dar es Salaam kuwa, kati ya halmashauri za wilaya 184 nchini, 90 kati ya hizo hazifanyi uchaguzi huo Novemba 24 mwaka huu kwa kuwa wagombea wamepita bila kupingwa.

“Katika mikoa 26 ya hapa bara, kwa taarifa ambazo tumeshapokea mpaka leo asubuhi mikoa mitatu inaonekana kwamba wagombea wa Chama Cha Mapinduzi wamepita bila kupingwa kwa hiyo kuanzia siku ya uteuzi wao ni viongozi halali na wasimamizi wameshawateua, hakuna haja ya kampeni katika eneo hilo” ameyasema hayo wakati anazungumza kwenye kipindi cha Asubuhi Hii kinachorushwa na kituo cha redio cha TBC Taifa cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Wakati akizungumza na Habarileo leo mchana Waitara ameitaja mikoa ambayo haitafanya uchaguzi kabisa kuwa ni Katavi, Tanga, na Ruvuma.

“Mahalali ambako mgombea alikuwa peke yake na amepita bila kupingwa kazi ya msimamizi ni kumtangaza na baada ya hapo atasubiri baada ya tarehe 24 ataapishwa na ataanza majukumu yake kwa hiyo hakuna habari ya kampeni lakini mikoa 23 itakuwa na mchakato wa uchaguzi”amesema.