Mkoa wa Manyara asilimia 79 wapo tayari kupiga Kura Novemba 24 mwaka huu


Na John Walter-Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema katika zoezi la uandikishaji daftari la kudumu la kupiga kura,mkoa wake umeandikisha watu 5,65,827 sawa na asilimia 79 ya lengo la kuandikisha watu 7,20,742.

Ameeleza hayo wakati akitoa taarifa ya zoezi la uandikishaji mbele ya Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo ambaye kwa sasa anapita katika mikoa yote Tanzania bara kuhakiki zoezi lilivyofanyika huku akitoa maagizo kwa kamati za rufaa zilizoundwa zikasikilize malalamiko ya watu waliokata rufaa na kutoa haki.

Mnyeti ameongeza kuwa wagombea wote walipewa uhuru wa kurejesha fomu kadri walivyoweza ukiachilia mbali ambao hawakuonekana  kabisa wakati wa urejeshaji wa fomu.

Chama cha Mapinduzi waliochukua fomu ni 11,621 na kurejesha 11, 516 ikiwa ni sawa na asilimia 96, Chadema walichukua fomu 3,175 na zilizorejeshwa ni 2,152 asilimia 68,Cuf wamechukua fomu 283  na kurejesha 78 sawa na asilimia 27,Nccr Mageuzi 100 wamechukua Fomu na 54 wamerejesha sawa na asilimia 54 huku Act Wazalendo waliochukua fomu wakiwa 38 na waliorejesha ni 34 ambayo ni asilimia 89.

Mkoa wa Manyara upo Kanda ya Kaskazini ambao unaundwa na wilaya tano za Mbulu,Babati,Kiteto,Simanjiro na Hanang,wananchi wake wamejitokeza kujiandikisha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa kuchagua viongozi wa serikali za Mitaa,Vijiji na vitongoji Novemba 24 mwaka huu.