Mradi wa kiwanda kikubwa cha dawa Tanzania wavutia Wawekezaji wa Kimkakati Afrika Kusini

Tanzania imewasilisha miradi 13 ya Kipaumbele kwa wawekezaji wa kimkakati wanaoshiriki kongamano la Jukwaa la Uwekezaji Mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango anayemwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Jukwaa hilo, amesema Mradi wa Ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa  mchanganyiko kitakachogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 408 umewavutia wawekezaji wengi.

Amewataja wawekezaji waliovutiwa na mradi  wa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachojengwa Kibaha mkoani Pwani, kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya aina 230 za dawa kwamba wanatoka nchi za Korea, Uturuki, taasisi za fedha za kimataifa na kwamba hadi kufika mapema mwakani (2020) mwekezaji mmoja au zaidi watakuwa wamepatikana kwa ajili ya kuanza kujenga mradi huo.

“Pamoja na kupunguza tatizo la uhaba wa dawa na dawa bandia zinazoingizwa nchini, kiwanda hiki pia kitazalisha ajira  kwa watanzania” alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango amesema Serikali inatenga zaidi ya sh bilioni 230 kwenye Bajeti kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa huku mahitaji halisi ya dawa nchini ni takriban shilingi trilioni 1.4 ndio maana mkazo umewekwa kwenye ujenzi wa kiwanda hicho kitakachotatua changamoto za upatikanaji wa dawa nchini.


Alifafanua kuwa miradi mingine 12 iliyowasilishwa mbele ya wawekezaji hao iko katika hatua za maandalizi na iko katika sekta za Nishati ya umeme unaotumia nguvu ya maji, viwanda vya kuchakata pamba ili kuiongezea thamani na hatimaye kuzalisha nguo, ambavyo vinaendana na dhamira ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka Bohari ya Dawa ya Taifa Mhandisi Fredrick Pondamali ameeleza kuwa usanifu wa mradi huo wa kiwanda cha kuzalisha dawa mchanganyiko umekamilika pamoja na viwanda vingine viwili zaidi vinavyotafutiwa wawekezaji.

Alisema kuwa mradi wa kiwanda cha kuzalisha dawa ulichaguliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa lengo la kuupeleka mbele ya wawekezaji ili uweze kupata fedha kutokana na umuhimu wake kwa Tanzania na nchi jirani.

Jukwaa hilo la Uwekezaji Afrika linalofanyika kwa mwaka wa pili sasa limeandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali ambapo mwaka huu limevuta wawekezaji wa kimkakati zaidi ya 4000 kutoka kila pembe ya dunia ikiwa na lengo la kuongeza uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ili kuchochea kasi ya mabadiliko ya kiuchumi katika nchi za Bara la Afrika.