Serikali kununua ndege ya mizigo


Serikali imesema imeshaanza mazungumzo ya namna ya kupata ndege ya mizigo kwaajili ya kubeba mazao ya mbogamboja kuyepaleka nje ili kuwasaidia wakula.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe Bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kutafuta ufumbuzi wa masoko ya mazao ya mbogamboga.

“Ni kwanini tusiangalie uwezekano kama nchi kununua ndege ya mizigo itakayosaidia wakulima wetu nje ya nchi kwasababu mazao haya ya mbogamboga yanakwenda Nairobi na kusafirishwa na ndege za Kenya,” amehoji.

Waziri Kamwelwe akijibu swali hilo amesema serikali imeshafanya mazungumzo juu ya suala hilo na kwamba wana mpango wa kuanza kukodisha ndege kwaajili ya kusafirisha mazao hayo na minofu ya samaki kutoka Mwanza.

“Tayari tuna miezi mitatu tulishaanza kujadiliana kuhusiana na jinsi ya kupata ndege ya mizigo kwaajili ya kubeba mazao ya hot culture Uwanja wa Ndege wa Songwe pamoja na minofu ya samaki kutoka Mwanza kwahiyo tutaanza na kukodi ndege kwasababu tuna changamoto ya mzigo wa kutoka Europe kuja huku lakini kutoka hapa kwenda kule mzigo upo,” amesema Kamwelwe.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema serikali imekuwa ikihamasisha wakulima na wadau wengine kuongeza uzalishaji wa zao la parachichi hususan aina ya hass, kutekeleza mkakati wa kuainisha maeneo yote yanayofaa kwa kilimo hicho nchini pamoja na kuongeza uzalishaji wa miche ya maparachichi aina ya hass na kuilinda ili isiharibiwe na aina nyingine za mapachichi.