https://monetag.com/?ref_id=TTIb Shilingi milioni 40 kutumika kwa ufuatiliaji wa fedha za umma katika miradi ya maji kata za wilaya ya Lindi | Muungwana BLOG

Shilingi milioni 40 kutumika kwa ufuatiliaji wa fedha za umma katika miradi ya maji kata za wilaya ya Lindi



Na Ahmad Mmow, Lindi.

Katika kuhakikisha wananchi wa kata za Nyangamara, Pangatena na Namangale wanapata uwezo wa kufuatilia matumizi ya rasilimali fedha za umma katika sekta ya maji katika kata za Namangale Pangatena na  Nyangamara. Jumla ya shilingi 40,000,000 zitatumika kuwajengea uwezo wananchi waweze kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maji iliyopo kwenye kata hizo.

Hayo yalielezwa juzi na mkurugenzi wa shirika la maendeleo la wanawake wa Rondo( ROWODO), Scholastica Nguli wakati wa hafla ya kutambulisha  mradi wa  ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma kwa viongozi na watendaji wa wilaya ya Lindi, ambayo ilifanyika Lindi mjini.

Nguli alisema mradi huo ambao utadumu kwa kipindi cha miezi saba kuanzia sasa, lengo lake nikuwawezesha wananchi wa kata hizo waweze kufuatilia matumizi ya fedha katika miradi ya maji inayotekelezwa kwenye kata hizo. Ambapo kiasi hicho cha fedha kitatumika kuwajengea uwezo wa kufuatilia.

Alisema wameamua kufuatilia matumizi ya fedha kwenye sekta ya maji ili kuunga mkono jitihada za serikali katika sekta hiyo muhimu, kufuatia mpango wake wa kutua ndoo wanawake  kichwani.

Alisema dhamira kuu ni uwajibikaji na uwazi wa vijiji na kata kuhusu michakato ya maendeleo, kuhamasisha jamii ishiriki kikamilifu uibuaji, utekelezaji kwa ufanisi mipango ya maendeleo katika maeneo yao na kuboresha usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya maji.

 '' Malengo mengine ni ushirikishaji wananchi katika kupanga matumizi ya fedha na rasilimali za umma kwenye sekta hiyo katika kata za mradi,'' alibainisha Nguli.

Mkurugenzi huyo aliweka wazi kwamba kuboreka kwa miundombinu ya maji katika kata hizo kutasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuimarika kwa uelewa wa wananchi hao katika kutimiza wajibu wao katika sekta hiyo.

 ''Pia kutakuwa na ukuaji wa dhamira ya watendaji wa serikali kwa kutoa taarifa za maendeleo kwa wananchi. Ikiwamo taarifa za mapato na matumizi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya miradi ya maji kwa ngazi za vijiji na kata,'' alisema.

Mradi huo wa ufuatiliaji ulitambulishwa kwa viongozi 39 na watendaji 39 wa ngazi ya wilaya ambao waliongozwa na mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga.