Washukiwa watatu wa kundi la IS wakamatwa

Maafisa nchini Ujerumani wamewakamata watu watatu wanaodaiwa kuwa waungaji mkono wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu leo kwa tuhuma za kutayarisha shambulio kubwa dhidi ya watu ambao si Waislamu.

Waendesha mashitaka mjini Frankfurt wamesema kiasi ya polisi 170 walifanya msako katika nyumba tatu katika mji wa karibu wa Offenbach na kuwakamata watu hao, ambao tayari wanafahamika na maafisa wa usalama.

Uingiliaji kati huo umefanyika katika muda muafaka kuzuwia kitisho halisi, mkuu wa idara ya waendesha mashitaka Nadja Niesen aliwaambia waandishi habari mjini Frankfurt.

Amesema washukiwa wanaonekana walikuwa wamepanga shambulio katika ukanda wa mito ya Rhine na Main kwa nia ya kuuwa watu wengi iwezekanavyo, wa kile kinachoelezwa kuwa wasio amini.

Lakini haifahamiki bado iwapo walikwisha chagua eneo maalum la kufanyia uhalifu huo.