Waziri Jafo asema hakuna atakayejitoa uchaguzi wa Serikali za Mitaa


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amesema hakuna atakayejitoa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wote waliochukua fomu na kurejesha watashiriki uchaguzi huo kasoro wenye makosa ya uraia, kutojiandikisha katika mtaa husika, kujiandikisha mara mbili, kutodhaminiwa na chama chake.

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusiana na mwenendo wa Uchaguzi huo.

“Tukutane tarehe 24 Novemba hakuna kuweka mpira kwapani, vyama vikapambane kuanzia tarehe 17 hadi 23 katika kampeni”  amesema Waziri Jafo.

Pia Waziri Jafo amesema kwenye mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mapingamizi ya rufaa yaliyopokelewa ni 15,380 na Novemba 9 jumla ya rufaa 4,921 zilipitishwa sawa na asilimia 32 na zilizobaki zilikosa sifa.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepita bila kupingwa katika vijiji 6,248 kati ya 12,319 mitaa 1,169 kati ya 4,263 na vitongoji 37,505 kati ya 64,384.