Bagamoyo waanzisha vita dhidi ya dawa za kulevya



Na Omary Mngindo, Bagamoyo

Serikali wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imeanzisha vita dhidi ya dawa za kulevya kwa vijana, ikiwa na lengo la kuwanusuru vijana waondokane na matumizi hayo.

Mkuu wa wilaya hiyo Zaynabu Kawawa mwishoni mwa wiki ameongoza uzinduzi wa mpango huo kwenye fukwe za Bahari ya Hindi zilizoko mjini hapa, ambapo amewaomba walengwa kuachana na dawa za kulevya kwani zinawaondolea utu wao.

"Vijana wenzangu niwaombe muachane na matumizi ya dawa za kulevya, kutokana na kujiingiza katika matumizi hayo mmekuwa mkitengwa na jamii kutokana na kujiingiza kwenye matumizi hayo," alisema Kawawa.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mradi huo Dr. Eric Aris alianza kuishukuru ofisi ya Mkuu huyo kwa kuukubali mpango huo, unaoratibiwa na Serikali ya watu wa Marekani, huku akisema kwamba wamejionea vijana waliobadilika kwa kuachana na matumizi ya dawa.

"Tulifika katika ofisi yako tukazungumzia kuhisiana na zoezi hili, tunakushukuru binafsi ukishirikiana na wataalamu wako mmeukubali mpango huu, na leo tuko hapa na vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya tumewaona," alisema Dr. Aris.

Mratibu wa dawa za kulevya wilayani Bagamoyo Husna Kipilipili amemweleza Mkuu huyo kwamba kikundi cha Umoja wa Vijana Walioacha Dawa za Kulevya Bagamoyo (UVIWAMABA) kimechaguliwa Kitaifa kuwa kikindi kitachowabaini vijana wanaitumia dawa hizo wilayani hapa.

"Mpango wetu wa kuwapatia huduma za dawa za Mesadol zitaanza rasmi wilayani Bagamoyo Jumatatu ya Des 16 kuanzia saa 11 alfajili, hatua hii itawapatia nafasi walengwa kuwa na muda wa kwenda kuendelea na shughuli zao za kujipatia kipato.

Awali Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Farh Mohamed ameishukuru taasisi ya MVH kwa kuona umuhimu wa kuwafikia kwa ajili ya kuwapatia elimu na tiba vijana waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya.