DC aagiza kila mtu kulima hekari mbili


Kila mkazi wa Wilaya ya Kaliua mwenye uwezo wa kufanya kazi, ametakiwa kuhakikisha analima ekari moja ya zao la chakula na nyingine ya zao la biashara msimu huu ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kutokomeza umaskini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Abel Busalama, katika ziara ya kuhimiza wananchi kushiriki katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara katika vijiji mbalimbali wilayani humo.

"Tunataka mwaka huu kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, alime ekari moja ya zao lolote la chakula na ekari nyingine alime zao lolote la biashara, ikiwa pamba sawa, ikiwa korosho sawa, na ikiwa tumbaku sawa," aliagiza.

Alisema mpango wa wilaya ni kuhakikisha wanahimiza kila mwanakaya mwenye uwezo wa kufanya kazi, anakuwa na shamba lisilopungua ekari mbili ikiwa na zao la chakula na biashara ili uzalishaji wa mazao hayo uongezeke na kuiwezesha halmashauri kupata mapato yanayotokana na mauzo ya mazao ya biashara.

Pia, aliwataka wakulima kutumia fursa iliyotolewa na serikali ya mkulima kutowekewa vikwazo katika uuzaji wa mazao yake.