Marekani kutoza ushuru bidhaa zinazotoka Brazil na Argentina

Rais Donald Trump ametangaza kuwa Marekani itatoza ushuru kwa bidhaa za chuma cha pua na alumini zinazoagizwa kutoka Brazil na Argentina.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Trump ameandika kwamba, Brazil na Argentina zimekuwa zikiongoza katika kuishusha thamani ya sarafu zao, akiongeza kuwa hatua hiyo inawaumiza wakulima wa Marekani.

Trump pia ameitaka benki kuu vivyo hivyo kuchukua hatua kama hizo ili mataifa mengine yasitumie vibaya uimara wa dola ya Marekani katika kuzishusha thamani sarafu za nchi zao.

Mwaka jana Trump alitangaza nyongeza ya ushuru wa asilimia 25 katika chuma cha pua na asilimia 10 katika alumini, lakini mwezi Machi alitangaza tena kuondoa ushuru huo hasa kwa nchi za Argentina na Brazil pamoja na nchi nyingine ambazo awali zilikuwa zimejumuishwa.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amesema atazungumza moja kwa moja na Trump juu ya hatua hiyo.