Eliud Kipchoge ajiandaa kutetea taji lake katika mbio za Olimpiki za Tokyo 2020


Mwanariadha anayeshika rekodi ya dunia mbio za marathon, Eliud Kipchoge, amepuuzilia mbali mipango ya kustaafu licha ya kuandikisha rekodi ya kumaliza mbio hizo chini ya saa mbili wakati wa kivumbi cha INEOS 1:59 Challenge jijini Vienna, Austria.

Badala yake, bingwa huyo kwa sasa anajianda kutetea taji lake katika mashindano ya mbio za Olimpiki mnamo Agosti, 2020, jijini Tokyo.

 Katika mahojiano na Reuters Kipchoge alisema mashindano ya Olimpiki ya 2020 ni moja ya mipango yake na ana azimia kushiriki endapo atachaguliwa.

Katika hatua ya kuepukana na joto kali na hali mbaya ya hewa eneo la Tokyo, Kamati ya Olimpiki Duniani (IOC) imeamua kuhamisha mashindano hayo hadi mjini Sapporo.