Malori yanayobeba mizigo na watu kukamatwa - OCD Kahama




Na Paschal Malulu-Kahama.

Kamanda wa jeshi la polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga Lutusyo Mwakyusa amewataka wamiliki wa magari ya kubeba mizigo ya Matofali, Mchanga, Moramu na Kokoto na madereva kuacha tabia ya kubeba mizigo hiyo pamoja na watu kitu ambacho ni uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.

Kauli hiyo imekuja baada ya wamiliki na madereva wa magari hayo kulitupia lawama jeshi la polisi usalama barabarani limekuwa likiwatoza faini za uchakavu wa gari wakishindwa kutambua mizigo inayobebwa ndio inayofanya kuchakaa kwa gari hilo.

Mmoja wa wachimbaji hao John Chacha amesema askari wa usalama barabarani wamekuwa kero kwani wamekuwa wakifika hadi viwandani kwenda kukagua magari kitu ambacho sio sahihi huku akiongeza kuwa aina ya mizigo wanayobeba katika magari yao ni lazima iambatane na watu wakuishusha lakini wamekuwa wakizuiwa.

Amesema kuna baadhi ya makosa mengine wanapaswa kuyaangalia ikiwemo la uchakavu wa gari kwani hali hiyo inasababishwa na shughuli hizo hivyo wanamuomba kamanda wa jeshi la polisi kulishughulikia suala hilo kwani linawaumiza kwa kiasi kikubwa.

Kamanda wa jeshi la polisi Lutusyo Mwkyusa amesema kwa jeshi la polisi linafanya kazi kwa mjibu wa sheria za nchi hivyo kupigwa faini gari ambayo imechakaa pamoja na kubeba watu hayo ni makosa kwani huwezi kuchanganya mizigo na watu.

Amesema kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani gari ambayo imechakaa haipaswi kuingia barabarani kwani inaweza kusababisha ajali kwa watu au magari mengine hivyo wahakikishe wanatunza magari yao kwa makini ili kuendana na taratibu za nchi.