Meya Sita avipongeza vyama vya Ushirika Kinondoni kwa kutoa vifaa vya Hospitali katika kituo cha Afya Kigogo

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita amevipongeza vyama vya ushirika vilivyopo katika Halmashauri hiyo kwa kujitolea vifaa vya Hospitali katika Kituo Cha Afya cha Kigogo.

Aidha vyama hivyo vimemkabidhi Mhe. Sita  Magodoro 30, mashuka na foronya  150 ambapo wamesema kuwa vitasaidia wagonjwa watakaokuwa wanapatiwa matibabu katika kituo hicho.


 Akizungumza na vyama hivyo kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Meya Sita amesema kuwa  vitasaidia kuwahudumia wananchi mbalimbali watakao kuwa wanapatiwa huduma katika Kituo hicho cha Afya na kuwasihi  wengine kujitokeze kuchangia.

Amefafanua kuwa suala la Afya ni pana na kwamba Halmashauri iliamua kujenga Kituo hicho cha Afya ili kuwezesha wananchi kupata huduma kwa haraka na urahisi kutoka maeneo mbalimbali.

Ameeleza kuwa, Halmashauri ya Kinondoni inahudumia watu kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Bagamoyo, na kwamba  kulingana na wingi huo, imeweza kununua eneo hilo na  kujenga Kituo hicho cha Afya na kwamba watu kutoka shemu mbalimbali watapata huduma safi na bora inayokidhi viwango.

 Ameongeza kuwa” Tumepambana usiku na mchana, na mpongeza sana Mkurugenzi wetu , Ndugu Aron Kagurumjuli na watendaji wote kwa kufanikisha ujenzi wa Kituo hichi cha Afya, ambacho kitahudumia watu sio Kigogo tu , bali kitatoa huduma Ilala, Ubungo, na maeneo mengine kama ilivyo kwa Kituo cha Afya cha Magomeni.” amesema Meya Sita.

Hata hivyo Mhe. Sita emesema “ ninawapongeza sana, ninaimani wadau wengine watakapo ona hivi, itawakumbusha kuona kwamba wanawajibu kufanya hivi kama walivyofanya hawa vyama vya ushirika kutambua umuhimu wa afya katika Halmashauri yetu” ameongeza.

Kwa upande wake  Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji, na Ushirika , Ndugu. Salehe Hija amekipongeza kitengo cha ushirika kwa kuandaa vifaa hivyo na kukabidhi katika Kituo hicho cha Afya na kusema kuwa kitendo hicho kitaonyesha njia  kwa watu wengine kujitolea.

Aidha Hija amesema kuwa vifaa hivyo vilivyotolewa vinathamani ya shilingi milioni 6.7 huku  kituo hicho kikiwa na uhitaji wa vitanda 150 ambapo  kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa Kituo hicho , magodoro hayo  yaliyotolewa ni ni sawa na asilimia 20 ya mahitaji hayo.