Serikali haitopanga bei elekezi kwenye Mazao - Waziri Hasunga


Serikali imesema kuwa haitopanga bei elekezi kwenye mazao mbalimbali ya kilimo kuanzia msimu ujao wa kilimo wa mwaka 2019/2020 badala yake itaacha soko liamue.


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Lindi wakati akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo kukagua hatua zilizofikiwa za malipo ya wakulima wa korosho msimu wa mwaka 2018/2019.

Waziri Hasunga amesema kuwa katika kipindi kirefu serikali imekuwa ikijihusisha kupanga bei elekezi ya mazao jambo ambalo huchochea sintofahamu kwa wakulima wakati bei ya mazao katika soko la Dunia inaposhuka.

Amesema kuwa serikali itahakikisha kuwa inasimamia kwa weledi sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uhalali katika biashara ya mazao ya wakulima kwa kuangalia mwenendo wa soko la Dunia, uwezo wa wanunuzi na kiasi kitakacholipwa kwa wakulima.

“Tumepanga bei huko kwenye Pamba tumekoswakoswa, Tukapanga kwenye kahawa mambo mabaya, kwenye tumbaku mambo mabaya, tumesema wakulima wenyewe wanapolima ndio wapange bei” Alisema Mhe Hasunga

Katika upande mwingine Waziri Hasunga amesema kuwa serikasli kupitia wizara ya Kilimo inajipanga kuhakikisha kuwa inawasimamia maafisa ugani kwa weledi mkubwa ili waweze kuwasaidia wakulima ili kuwa na uzalishaji wenye tija.

Amesema kuwa wizara imekusudia kuweka utaratibu utakaowawezesha maafisa ugani hao kuwa na fomu maalumu zitakazopima utendaji kazi wao.

Hasunga amesema kuwa ofisi za maafisa ugani ni mashambani hivyo  ni lazima wapimwe ufanisi wao wa kazi kwa kwenda mashambani na jinsi walivyowasaidia wakulima.

Kwa upande mwingine waziri Hasunga amezitaja taasisi za fedha kutofanya vizuri katika kuwasaidia wakulima ili kupata mikopo yenye riba nafuu jambo litakalowanufaisha na kuongeza uwezekano wa kuwa na zana bora za kilimo kadhalika pembejeo bora.

Katika ziara hiyo Waziri Hasunga amebaini baadhi ya wakulima waliouza korosho zao kwa serikali katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 kutolipwa fedha zao jambo ambalo limemshangaza Kwakuwa serikali ilishatoa fedha zote kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao.