Serikali kujenga chuo cha VETA Masasi



Na Hamisi Abdurahmani, Masasi

Serikali imeweka wazi kuwa iko mbioni kujenga Chuo Cha mafunzo ufundi stadi (VETA) wilayani Masasi Mkoani Mtwara lengo ni kupanua fursa za upatikanaji wa ujuzi wa ufundi stadi kwa vijana  wa mikoa ya kusini.

  Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki wilayani Masasi na Mkuu wa wilaya ya Masasi, Selemani Mzee wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilayani hiyo kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya mgambo.

 Mzee alisema serikali kupitia wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia katika bajeti ya mwaka 2019/ 2020 ilitenga fedha kiasi cha sh.bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya mafunzo stadi VETA 25 kwenye wilaya mbalimbali nchini.

  Alisema miongoni mwa wilaya hizo wilaya ya Masasi inatarajia kunufaika na mpango huo wa kujengewa chuo cha VETA ni pamoja na wilaya ya Masasi.

 Mzee alisema serikali iliiagiza serikali ya wilaya ya Masasi kutafuta eneo ambalo ujenzi huo utafanyika na kwamba tayari eneo hilo limeshapatikana na kinachosubiliwa kwa sasa ni kuanza hatua za awali za ujenzi.

  Alisema wananchi wa kata ya Chikundi kijiji cha Msigalila wametoa bure eneo la jumla ya hekari 50 ili kupisha ujenzi huo wa chuo cha VETA Masasi.

  Alisema eneo hilo wananchi hao wameamua kulitoa baada ya kusikia serikali imetenga bajeti ya kutaka kujenga ujenzi wa chuo hicho.

   Alisema wilaya ya Masasi inazalisha vijana wengi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari hivyo ujenzi wa chuo itakuwa fursa pekee kwa wale vijana ambao hawatabahatika kuingia elimu ya chuo kikuu na serikali kupata ufundi stadi.

"Sisi wilaya ya Masasi tunamshukuru raisi Dk. John Magufuli kwa adhima hii ya kutaka kutujengea chuo hiki cha VETA Masasi pia tunawashukuru wananchi waliotoa eneo hili ili kupisha ujenzi," alisema Mzee

  Alisema serikali wilaya ya Masasi inaamini kuwa vijana wengi wilayani humo watanufaika na chuo hicho kwa kupata elimu itakayokuwa inatolewa hivyo wazazi na vijana wenyewe waitumie fursa hiyo.

  Baadhi ya wananchi wilayani humo waliohojiwa  kuhusu fursa ya uwepo wa chuo cha VETA tarajiwa, akiwaemo Mustapha Sadi na Fatuma Marijani, walisema wanaipongeza serikali kwa hatua hiyo mzuri.

  Walisema kuwa chuo hicho kitawakomboa vijana wengi wa wilaya za kusini ambao wamekuwa wakikosa nafasi za kuendelea na masomo ya chuo kikuu au sekondari.