TAKUKURU, Skauti kutoa elimu ya rushwa Shuleni


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, amekitaka Chama cha Skauti Tanzania kuanzisha miradi ya kilimo cha mboga mboga kwa lengo la kuinua kipato na kuwawezesha vijana wa chama hicho kuwa na uelewa wa kufanya kazi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Desemba 4, 2019, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho amesema uanzishwaji wa mradi huo utawajengea vijana hao utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii.

Prof. Ndalichako amesema uongozi wa chama hicho ukiwa na ubunifu na nia thabiti ya kukabiliana na changamoto hakika vijana watajifunza mambo mengi mazuri na namna ya kujenga taifa lao kwa ari moja.

"Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuwafundisha vijana hao na kuwapatia elimu ambayo inawafanya watambue mambo ambayo hayafai katika taifa hili likiwamo suala la rushwa," amesema Prof. Ndalichako.

Aidha amewataka wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao kujiunga na chama hicho kwani kimekuwa kikiwafundisha vijana maadili mema na kupinga rushwa.

Awali Mkuu wa Skauti Tanzania, Mwantumi Mahiza, amesema kuwa ili kutatua tatizo la rushwa nchini hasa kwa kuwaandaa vijana tayari wameingia makubaliano na Taasisi ya kuthibiti na kupamba na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), kutoa elimu kupitia skauti katika shule za msingi na sekondari nchini.