Wachimbaji Mchanga na waponda Kokoto kuhamishwa



Na Paschal Malulu-Kahama.

Wachimbaji wa madini ujenzi katika halmashauri ya mji wa Kahama wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameiomba ofisi ya kamishina wa madini mkoa wa Shinyanga kusitisha mpango wa kuwaondoa wachimbaji hao katika maeneo wanayofanyia kazi na kuwarasimisha katika maeneo waliyopo.

Wakizungumza katika kikao cha wachimbaji madini ujenzi kikiongozwa na kamishina wa madini mkoa wa Shinyanga wachimbaji hao wamesema maeneo waliyopangiwa na halmashauri sio rafiki kwani ni mbali kwa usafirishaji madini hayo hivyo halmashauri kupitia kwa kamishina wanaomba wapatiwe leseni ya uchimbaji na maeneo yao waendelee kuyatumia kuchimba.

Mwenyekiti wa wachimbaji hao Martin Clemence amesema katika halmashauri ya mji wa Kahama wana vituo vitatu vya kuegesha magari ya usombaji madini hayo ya Mchanga, Moramu, Mawe na Kokoto hivyo kuhamishwa kwa maeneo ambayo kwa sasa wanayatumia na kuelekezwa eneo moja gharama ya usafirishaji itapanda na kusababisha ujenzi wa nyumba kuwa mgumu.

Amesema wao kama wachimbaji na wasafirishaji wanaiomba ofisi ya kamishina mkoa kuwatambua kwa kuwapatia leseni pamoja na ofisi hiyo kukagua maeneo ya uzalishaji Mchanga na Kokoto ili kujiridhisha kiusalama na kuruhusu kuendelea na shughuli za uchimbaji kwani kwenda maeneo yaliyotengwa ni zaidi ya KM 50.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi halmashauri ya mji wa Kahama Johanes Mwebesa amesema halmashauri ya mji imetenga maeneo matatu ya uchimbaji wa Mchanga, upondaji wa Kokoto na Mawe miongoni ni Ngogwa na Wendele hivyo kinachosubiriwa ni utaratibu kutoka ofisi ya madini.

Kwa upande wake kamishina wa madini mkoa wa Shinyanga Joseph Kumbulu amesema wachimbaji na waponda kokoto walio na leseni hawatahamishwa isipokuwa watakaohamishwa ni wale wasio kuwa na leseni sambamba na walio maeneo yasiyokuwa salama kwa shughuli za uchimbaji na uvunjani Mawe.

Aidha amesema wachimabaji walio na maeneo yao binafsi idara zinazohusika ikiwemo mazingira watafika na kujiridhisha huku wale wote wanaofanya shughuli hizo ndani ya mji wataondolewa na kupelekwa katika maeneo yaliyotengwa na halmashauri huku akisisitiza wachimbaji wote lazima wapatiwe leseni.