Waziri Hasunga apiga marufuku visima kuchimbwa kwa gharama ya zaidi ya mil 20 wilayani Mtwara



Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kubadili matumizi ya gharama za uchimbaji wa visima kutoka Tsh Milioni 160 mpaka kuchimba kwa Tsh Milioni 20.

Waziri Hasunga ametoa agizo hilo tarehe 14 Disemba 2019 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea skimu ya umwagiliaji ya Kitere iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Amesema kuwa gharama za uchimbaji wa kisima kimoja kwa ajili ya umwagiliaji haipaswi kuzidi shilingi Milioni 20 kwani kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu na kushindwa kuakisi kasi ya utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.


Katika ziara hiyo Waziri Hasunga ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuchimba visima vitatu katika eneo hilo kwa kiasi cha shilingi milioni 60 ikiwa ni shilingi milioni 20 kwa kila kisima kimoja.

Amesema kuwa umefika wakati wa wakulima kuachana na kilimo cha kutegemea mvua za msimu badala yake kuhakikisha kuwa wanalima kilimo bora cha umwagiliaji.

Kadhalika amekumbushia agizo lake alilolitoa hivi karibuni la kila mkoa kuwa na Afisa umwagiliaji wa mkoa huku wilaya zote zenye skimu za umwagiliaji kuwa na afisa umwagiliaji wa wilaya.

Waziri Hasunga amesema kuwa mkakati huo madhubuti wa serikali kuhakikisha kunakuwa na skimu nyingi za umwagiliaji utaimarisha sekta ya kilimo jambo litakaloongeza kipato cha mtu mmoja mmoja sambamba na Taifa kwa ujumla wake.

Kuhusu mkakati wa serikali kuwa na kiasi kikubwa cha umwagiliaji, ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ndani ya kipindi cha miaka miwili kuongeza eneo la umwagiliaji ili kufikia hekta milioni moja huku kakiongeza kuwa hadi kufikia mwaka 2025 eneo la umwagiliaji liwe limefikia Hekta milioni tano.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Evod Mmanda amewapongeza wakulima wa skimu hiyo kwa kuimarisha sekta ya kilimo huku akisisitiza kuwa serikali inapaswa kuongeza mkakati madhubuti wa kuimarisha masoko ya mazao ya wakulima.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Halmashauri Wilaya ya Mtwara Ndg Joseph Tesha akitoa taarifa fupi mbele ya Waziri wa Kilimo amesema kuwa skimu hiyo ya Kitere iliyopo katika kata ya Kitere inayohudumia vijiji vya Lilido na Chemchem ina jumla ya eneo la Hekta 920 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji huku eneo lililoendelezwa likiwa ni jumla ya Hekta 310 pekee.


Waziri Hasunga yupo mkoani Mtwara kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo awali alitembelea mkoa wa Pwani na Lindi kwa ajili ya kukagua hali ya uuzaji wa korosho msimu wa 2019/2020, kukagua hatua zilizofikiwa za malipo ya wakulima wa korosho zilizonunuliwa na serikali msimu wa mwaka 2018/2019 na kukagua skimu za umwagiliaji.