Waziri Jafo atoa agizo kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe



Na Amiri kilagalila-Njombe

Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa tamisemi Selemani Jafo amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kusimamia ukamilishwaji wa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo kutokana na kushindwa kukamilika kwa wakati na kupita muda uliopangwa.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo wilayani hapo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo na kukuta maendeleo ya ujenzi ukisuasua wakati hospitali nyingine za wilaya nchini zimekamilika.

“Mheshimiwa Rais alikwenda kuweka jiwe la Msingi hospitali ya Nkasi  jiografia ya Nkasi iliyopo mkoani Rukwa na wewe wa Wanging’ombe ni vitu viwili tofauti,kwanini Nkasi tumeweka jiwe la msingi hospitali majengo yote yamekamilika ninyi hapa hamjakamilisha,kwanini tumeenda kuweka jiwe la msingi hospitali ya Tanganyika majengo yote yamekamilika kwa asilimia mia moja ninyi hapa bado tena mumeweka ongezeko la milioni mia tano arobaini”Aliuliza waziri Jafo.


Kwa upande wake Injinia wa mradi huo Bonifas Kasambo,amesema miongoni mwa sababu za kuchelewa kukamilika kwa mradi ni pamoja na matumizi ya fedha ya mapato ya ndani kutokana na kuishiwa kwa fedha za mradi.

“Kumekuwa na kusua sua kutokana na kutumia fedha ya mapato ya ndani na fedha hii inapatikana kidogo kidogo,hivyo tumekuwa tunaenda taratibu sana”alisema Bonifas  Kasambo.


Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe Edes Lukoa amesema changamoto zilizosababisha mradi huo kusuasua ni pamoja upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kwa baadhi ya nyakati hivyo kuchelewesha kasi ya ujenzi.

Kutokana na maelezo hayo Waziri Jafo ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa hospitali hiyo.

“Hapa sijaridhika japo kazi imeonekana,inawezekana taratibu zenu za manunuzi hazikwenda vizuri ama kuna shida yoyote ile,ninachotaka ni kwamba mkurugenzi simamia majengo yakamilike haya ndio maelekezo yangu”

Aidha Waziri Jafo amesema serikali itafikishe shilingi milioni mia tano nyingine kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu,hiyo hatukusudii kwa ajili ya gepu zilizopo.


Mradi huo ulianza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2018-2019 kwa fedha kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kuanzia februali 11,2019 ikiwa ni miongoni mwa halmashauri 67 Tanzania bara zilizopewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba na kutakiwa kukamilika kwa ujenzi Octoba 30,2019