Agizo la mkuu wa Wilaya ya Kahama laanza kutekelezwa na wananchi



Na Paschal Malulu-Kahama

Wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameanza kutekeleza agizo la serikali la kusafisha mitaro ya maji taka inayowazunguka kwenye makazi yao ikiwemo na kuondoa michanga iliyoziba mitaro.

Wakati wakitekeleza agizo hilo la serikali baadhi ya wakazi wa mji wa Kahama waliopo kando ya mitaro hiyo wamesema hali hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kwani maji yataweza kupita kwa urahisi na mitaro kuwa misafi muda wote.

Robert Kalolo amesema kwa sasa halmashauri wanaiomba kuhakikisha inafanya mpango mkakati wa kuboresha miundombinu ya barabara kwani mchanga wote unaopita kwenye mitaro na kusababisha kuziba haitokei kwenye mitaro hiyo.

Amesema mitaro inayoziba inatokana na  baadhi ya maeneo miundombinu ya barabara sio mizuri hivyo pia mchanga unaotolewa kwenye mitaro iondolewe kwa wakati kwani kwa sasa inawekwa kando ya barabara ambapo mvua bado zinaendelea kunyesha hivyo mchanga huo unarudishwa kwenye mitaro.

Agizo hilo lilitolewa na mkuu wa wilaya ya Kahama Januari 20, 2020 Anamringi Macha kuwa kila mwananchi na mkazi wa wilayani humo kuhakikisha anazibua mitaro kwenye eneo lake na mtu yeyote atakaekaidi amri hiyo maduka makazi yake na sehemu yoyote inayomzunguka itafungiwa hadi atakapohakikisha amefanya usafi.

Alisema muda wa siku tatu unawatosha kufanya usafi wa mitaro kwenye maeneo yao hivyo siku yoyote atapita kwa ajili ya ukaguzi na kila mtu atachukuliwa hatua ambaye atakuwa hajatekeleza agizo hilo.

Aidha wananchi hao wameiomba serikali ya mji wa Kahama kubuni mbinu mbadala ya kuhakikisha mitaro hiyo haingiliwi na mchanga ambao unaonekana kuwa kero kuziba mitaro na kusababisha barabara kuharibiwa na mvua.