https://monetag.com/?ref_id=TTIb Ayoub awataka wawekezaji kuzingatia sheria na wajibu wao kwa jamii | Muungwana BLOG

Ayoub awataka wawekezaji kuzingatia sheria na wajibu wao kwa jamii



Na Thabit Madai,Zanzbar.

Wawekezaji nchini wametakiwa kuzingatia sheria za nchi na kutimiza wajibu wao kwa nchi na jamii inayowazunguka ili kuiimarisha sekta hiyo.

Akifungua na wawekezaji wa sekta mbali mbali zilizomo ndani ya mkoa wa Kusini Unguja katika ukumbi wa Chuo kikuu cha taifa Zanzibar (SUZA), Mkuu wa mkoa huo Ayoub Mohammed Mahmoud alisema kufanya hivyo kutachochea kasi ya maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema wawekezaji wamekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na kuimarisha ujuzi kutokana na shughuli wanazoziendesha, hivyo nia ya mkoa wake ni kuwafanya wawe imara zaidi ili waongeze mchango wao katika uchumi.

“Lengo la kukutana hapa ni kuona ni kwa namna gani tunaweza kuendeleza dhana ya uwekezaji kwa manufaa ya pande zote, serikali, jamii na nyinyi kwani mmekuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya nchi yetu na watu wake, “ alieleza Ayoub.

Aidha aliwaomba wawekezaji hao kuzitumia ofisi za wakuu wa wilaya na taasisi nyengine za serikali ili kurahishisha upatikanaji wa huduma zinazohusu shughuli zao hususani swala la umiliki wa ardhi.

“Katika swala la ardhi niwaombe msiwatumie watu wa katikati au madalali kwani tumegundusa kuwa ndio chjanzo cha migogoro mingi ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya mkoa wetu. Ni vyema mkazitumia ofisi zetu lakini pia taasisi zinazohusiana na ardhi kupata huduma ili kuepukana na migogoro isiyo ya lazima,” alieleza Mkuu huyo wa mkoa.

Kuhusu swala la usalama ambalo lilielezwa na wawekezaji hao kama moja ya changamoto inayowakabili, alieleza kuwa ipo haja ya kuwa na mpango wa pamoja wa ushirikiano utakaoongeza hali ya usalama kwa wageni na wenyeji wanaotumia huduma zinazotolewa na wawekezaji hao.

“Katika mkoa wetu kuna hoteli za kitalii na taasisi nyengine zinazotoa huduma kwa wageni zaidi ya 200. Hii ni nguvu kubwa tunayoweza kuitumia kustawisha ulinzi na usalama sio kwa kuongeza vituo vya polisi tuu bali pia kuweka mifumo ya ulinzi,” alisema.

Aidha aliwapongeza wawekezaji hao kwa kuamua kuwekeza katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo na kuwaomba kuendelea kushirikiana na wenyeji ili dhana ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) iwe na tija kwa jamii badala ya watu wachache.

Awali wawekezajio hao ambao wengi wao walitoka katika sekta ya utalii walimueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa pamoja na mafanuikio waliyonayo bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za usalama, uchafu wa mazingira hasa ya fukwe na vitisho vya baadhi ya watendaji wa sekta za serikali wanaokwenda kupata taarifa za maendeleo au shughuli zao.

Walieleza kuwa kuna baadhi ya watendaji wa taasisi za serikali wanapokwenda katika maeneo yao hawatumii lugha nzuri au kufuata taratibu jambo ambalo linapelekea mikwaruzano baina yao na wakuu wa hoteli.

“Watendaji wa baadhi ya taasisi za serikali hasa ZRB (bodi ya mapato) wanapokuja na kutukuta tupo katika majukumu yetu kwa wateja wanalazimisha wahudumiwe wao na unapojaribu kuwaomba wasubiri wanakutisha au wakati mwengine kushirtakiwa kuwa umewazuia wasitekeleze wajibu wao,” alieleza Innocent Chuma kutoka Sultan Palace.

Aidha walieleza kuwepo kwea taasisi zaidi ya moja katika masuala yta ukusanyaji wa tozo na kodi mbali mbali kunaleta mkanganyiko hivyo walishauri kuwepo kwa taasisis moja itakayokusanya kodi kwa uwakala wa taasisi nyengine badala ya kila taasisi kwenda kwa wakati wake.

Wakizungumza kwa wakati tofauti wakuu wa wilaya za mkoa huo Hamida Khamis Mussa (Kati) na Mustafa Kitwana Mustafa (Kusini Unguja) waliwashukuru wawekezaji hao na kumpongeza Mkuu huyo wa mkoa kwa kuamua kuitisha mkutano huo ambao ulihuduriwa pia na wawakilishi kutoka ZIPA, Kamisheni ya kazi, kamisheni ya utalii na wadaui wengine wakiwemo wawakilishi kutoka vyuo vikuu viliomo mkoani humo.

Walisema hatua hiyo itaimarisha uhusiano mwema uliopo kati ya wawekezazaji na serikali zao na kwamba katika kutatua baadhi ya changamoto, wameanza kuwasajili wadau wote wanaoendesha biashara katika fukwe za bahari za ukanda huo.

“Hatua ya kuwasajili imelenga kuwatambua na shughuli wanazoendesha ili iwe rahisi kuwafuatilia kwani wapo baadhi yao sio wazuri na ndio wanaojihusisha na vitendo viovu vikiwemo vya wizi na unyang’anyi,” alisema Hamida Mkuu wa wilaya ya Kati.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo ulilenga kuwakutanisha wawekezaji hao, watoa huduma na wazalishaji wa bidhaa zinazotumika katika mahoteli ili kuogeza tija na mapato ya taasisi zao jambo ambalo limepongezwa na kila mshiriki.