Bodi ya Nishati Vijijini(REB) yaagiza wazalishaji wa nyaya za umeme kusambaza haraka katika Miradi



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Julius Kalolo ameagiza wazalishaji wa nyaya za umeme zinazotumika katika Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza (REA III) kukamilisha usambazaji wa nyaya katika maeneo yote ya mradi kabla ya utekelezaji wa mradi mwezi Februari, mwaka huu.

Agizo hilo alilitoa katika ziara ya siku moja iliyofanyika tarehe 18/01/2020 katika viwanda vinavyotengeneza vifaa vya umeme vya Kilimanjaro Cables, MCL na Europe Industries (Tropical) vilivyopo Dar es Salaam.

Amesema wakandarasi wanadai kuwa wazalishaji wanashindwa kuzalisha nyaya kwa muda unaotakiwa kutokana na kuwa na zabuni nyingi.

Mwenyekiti huyo amesema lengo la ziara hiyo ni kukutana na watengenezaji wa nyaya na kukubaliana namna bora ya kutatua tatizo la uhaba wa nyaya.

Amesema kuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa Mradi hivi sasa ni kukosekana kwa nyaya ambazo zinahitajika kuwekwa ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya nishati ya umeme.

“Kwa upande wa MCL wanasema wana oda za kutosha hivyo hawawezi kupokea kwa muda huu mfupi oda mpya na kuzalisha kwa muda mfupi, lakini zile oda walizokuwa nazo wamesema hadi kufikia mwezi wa Februari watakuwa wamewapa wakandarasi ili wamalizie mradi,”amesema

Aidha, amesema Tropical wanasema hawana oda kutoka kwa wakandarasi wa REA zaidi ya Tanesco.

“Nyaya zipo lakini tatizo ni wakandarasi wetu, tunalishughulikia maana wana tatizo la kurundikana kwa mzalishaji mmoja,”amesema

Naye, Mkurugenzi wa Europe Industry Bw.Charles Mlawa ametoa rai kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuwa nyaya na transfoma zipo za kutosha na watatoa ushirikiano ili miradi ikamilike kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Nishati Vijijini, Mhandisi Styden Rwebangira, amesema katika maeneo ya vijijini waliyotembelea wamebaini nguzo kusimama kwa muda mrefu na taarifa zilizopo tatizo ni nyaya na kuwa wamepokea malalamiko kutoka kwa wakuu wa wilaya mikoa, wabunge madiwani na wananchi ambao hawajafikishiwa huduma ya umeme.

Mhandisi Rwebangira alisema Serikali imewapatia fursa wenye kwa kuzuia uagizaji wa nyaya toka nje ya nchi hivyo ni vema wakadhihirisha uwezo na wasitumie fursa hiyo kupandisha bei mara kwa mara.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amosi Maganga, amesema wamebaini kuwa baadhi ya wakandarasi wametoa oda za nyaya kwa viwanda vichache wakati vingine havina oda kutoka kwa wakandarasi wa REA.

Pia amesema mradi huo ulitarajiwa kukamilika Desemba mwaka jana lakini kutokana na sababu mbalimbali baadhi ya wakandarasi wapo asilimia 98 ya utekelezaji wengine 100 ni imani yangu kwa kipindi kilichobaki watakamilisha