Dk Shein ajidhatiti kulinda Amani na utulivu uliopo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema Serikali itahakikisha kwamba amani iliyopo inalindwa na kutunzwa kupitia vikosi vyake vya ulinzi na usalama vilivyopo nchini.

Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein huko Maisara mara baada ya kupokea amsha amsha ya vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopo Tanzania ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.


Amesema lengo la maonyesho hayo ya amsha amsha ni kuonyesha vyombo vinavyotumika katika vikosi vya ulinzi na usalama na jinsi wapiganaji wanavyojiandaa katika kulinda amani nchini.

Aidha Dkt. Shein ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaongozwa kwa kufuata sheria hivyo wananchi wote wanatakiwa kufuata sheria zilizowekwa nchini ili kudumisha amani na utulivu kwani vikosi vya ulinzi vinaendelea kulinda amani iliyopo.


“Kutokana na amani iliyopo nchini idadi ya watalii imezidi kuongezeka hadi kufikia 540,000 kwa mwaka uliopita, tunawaomba wageni wanaotaka kuitembelea Tanzania waje kwa wingi kwani nchi ina amani na na ulinzi upo wa kutosha”, ameeleza Dk. Shein.

Aidha Rais Dk. Shein amewaasa wale wote wanaohamasisha vurugu kuacha tabia hiyo kwani Serikali imejipanga kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na kuwachukulia hatua za kisheria kwa atakae kwenda kinyume na sheria za nchi.


Jumla ya vikosi tisa vya ulinzi na usalama vimeshiriki katika kuonyesha utayari wao wa kulinda amani na usalama wa nchi pamoja na kuyalinda na kuyaendeleza Mapinduzi ya Zanzibar.