Latu: Bagamoyo yaidhinisha bajeti ya Sh. Bil 34.4 kwa mwaka 2020/2021

Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ,imeidhinisha na kukadiria kutumia sh.bilioni 34.4 ,kwa ajili ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo ,mishahara ya watumishi na matumizi mengine ,katika kipindi cha mwaka 2020-2021.

Aidha, kiasi cha sh.bilioni 3.4 itatokana na mapato ya ndani kupitia vyanzo vyake vya mapato hayo.
Akizungumzia kuhusiana na bajeti hiyo wakati wa baraza maalum la madiwani, mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo ,Fatuma Latu alisema katika kiasi hicho cha fedha ,sh.milioni 844,816 .7 ni makadirio kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na uendeshaji wa idara na vitengo vya kamati ya uchumi,ujenzi na mazingira .

Aidha alifafanua kwamba,sh.bilioni 28.794.7 ni makadirio ya idara na vitengo vya kamati ya fedha ,uongozi na mipango.

Pamoja na hayo, upande wa elimu, afya na maji ni sh. bilioni 4.426.797.036.

“Lengo letu ni kufikia ama kupita malengo hayo tuliyojiwekea”alisema Fatuma.

Fatuma alitaja, mkakati wa waliojiwekea  ni kusisitiza usimamiaji wa vyanzo vya mapato ya machimbo ya mchanga,uvuvi na kutoa elimu sahihi ya matumizi ya machine za posi ili kudhibiti wizi wa mapato katika makusanyo.

“Utafiti ulifanywa kwa machimbo yasiyo rasmi ya mchanga na kokoto ambayo yanasababisha upotevu mkubwa wa fedha,tumeongea na watendaji wafanye tathmini ili kuweza kiyarasimisha na halmashauri iweze kujipatia kipato”alibainisha Fatuma.

Nao baadhi ya madiwani akiwemo diwani wa kata ya Makurunge Kabile na diwani wa Magomeni Mwanaharusi Jarufu walisema, ushirikiano ndio jambo kubwa ,kwani utasaidia kubaini mianya ya wizi kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato na kuifanyia kazi ili mapato yasiweze kupotea.

Nae diwani wa viti maalum tarafa ya Mwambao Shumina Rashid alisema , miundombinu ya barabara ikiboreshwa hasa kuelekea katika machimbo ya mchanga itawezesha barabara kupitika na kukusanya mapato kwa kiasi kikubwa kwani kati ya vyanzo vikuu wanavyovitegemea ni pamoja na machimbo ya mchanga na kokoto.