Marekani kupeleka wanajeshi wa ziada mashariki ya kati

Marekani inatuma maelfu ya wanajeshi wa ziada nchini Kuwait kwa lengo la kuongeza nguvu katika eneo hilo la Mashariki ya Kati kutokana na kuzidi mvutano baada ya Marekani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran.

Msemaji wa kamandi nambari 82 ya jeshi la Marekani, Mike Burns, amesema wanajeshi 3,500 watawasili Kuwait katika kipindi cha siku chache zijazo kujiunga na wengine 700 waliowasili mapema wiki hii.

Nyongeza ya wanajeshi inafuatia wasiwasi wa hatua za kulipa kisasi ambazo Iran inaweza kuchukua baada ya mashambulizi ya siku ya ijumaa yaliyomuua Jenerali Soleimani.

Soleimani, aliyekuwa kiongozi wa kikosi cha Quds kilicho chini ya kikosi kipana cha walinzi wa mapinduzi ya Iran, alikuwa akilaumiwa kwa miongo kadhaa kuratibu mashambulizi dhidi ya wanajeshi na Marekani na washirika wake katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati.