Mataifa yaliyopoteza raia kwenye ndege ya Ukraine yaidai fidia Iran

Mataifa yaliyopoteza raia katika ajali ya ndege ya Ukraine iliyodunguliwa na Iran yameitaka Tehran iwajibike kikamilifu, uchunguzi wa kimataifa uanzishwe na familia za wahanga zilipwe fidia.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Canada, Uingereza, Ukraine, Sweden, Uholanzi na Afghanistan wamekutana jijini London katika ubolozi wa Canada.

Mawaziri hao baada ya mkutano wao walitoa taarifa ya pamoja wakiitaka Iran ifanye uchunguzi wa kimataifa utakao kuwa huru na wazi hasa kwa mataifa yanayoomboleza.

Waziri wa mambo ya nje wa Canada Francois-Philippe Champagne amesema wamekutana  kutafuta uwajibikaji na haki kwa wahanga wa mkasa huo na kuongeza kuwa familia za wahanga hao zinataka majibu, jamii ya kimataifa inataka majibu na dunia nzima pia inasubiri majibu na kwamba hawatapumzika hadi watakapoyapata.Watu wote 176 waliokuwa wameabiri ndege ya abiria ya Ukraine walipoteza maisha yao wakati ndege yao ilipodunguliwa na kombora muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran tarehe 8 mwezi huu.