Mbunge Giga avitaka vyombo vinavyosimamia haki kusimamia ipasavyo Sheria



Na Thabit Madai,Zanzibar.

Mbunge wa Viti Maalumu Jumuiya ya Wazazi Tanzania,Najma Murtaza Giga amevitaka vyombo vinavyosimamia haki Ikiwemo Jeshi la Polisi na Ofisi ya  Mkurugenzi wa Mashtaka kusimamia vyema Sheria zilizowepo Nchini  ili kutoa ulinzi kwa watoto  wasidhalilishwe.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Mwandishi wetu kuhusu hatua Zinazochukuliwa na Jumuiya ya Wazazi katika ukabiliana na vitendo vya Udhalilishaji na unyanyasaji kwa watoto Nchini.

Mbunge huyo  alisema kwamba vyombo hivyo vinatakiwa kutekeleza ipasavyo  sheria hizo  kama vile Sheria namba 6  ya mwaka 2011 ambayo imeweka mazingira mazuri katika ulinzi wa watoto pamoja na kutoa maelekezo juu ya watoto ambao wamefanya makosa.

Giga alifahamisha kwamba Serikali imeshaweka mazingira mazuri katika ulinzi wa watoto hivyo vyombo vinavyosimamia haki vinatakiwa kuunga mkono hatua hizo za Serikali kwa kusimaia Sheria na taratibu mbali mbali ili watoto wasidhalilishwe.

“Sheria nzuri nzuri zimeshatungwa kwa lengo la kuwaweka watoto wetu katika Mazingira mazuri  lakini bila vyombo hivyi vya kutunga Sheria kuzisimamia na kutekeleza vyema watoto hawawezi kuwa salama” alisema Mbunge Najma Giga.

Alieleza katika kusimamia Sheria hizo jamii, wazazi, walezi , walimu pia wanatakiwa kuweka mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha watoto wanalindwa na kuwa Salama.

Hata hivyo Mbunge Giga aliwataka Jeshi la Polisi, Mawakili binafsi na Waserikali, Mahakama na Madaktari kurudi katika Imani na utamaduni wa Taifa letu kwa kukatas Rushwa ya Muhali.

“Kitu ambacho kinatutafuta kila siku na suala hili la Udhalilishaji liwe linazidi kuota mizizi ni kutokana na Rushwa ya muhali, tukiachana nayo basi watoto wetu watabakia Salama” alisema Giga.

Aliongeza kueeza kwamba adui mkubwa anayesababisha kukithiri kwa vitendo hivyo vya kinyama kwa watoto visiweze kumalizika ni Rushwa na Muhali ambao unaonekana umekukua kwa kiasi.

“Tunatakiwa kupinga kwa nguvu zote Rushwa na Muhali ili kukomesha vitendo hivi vya udhalilishaji” Alisema Mbunge huyo.

Katika Maelezo yake Mbunge huyo alisema Jumuiya ya wazazi ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM kinaungana na wadau wote pamoja na Serikali  katika kupiga vita suala la udhalilishaji wa watoto ambao umeota mizizi.

“Sisi kama wazazi tunaungana na Taasisi zote katika kupambana na suala hili la udhalilishaji kwani ni changamoto ambayo sisi kama wazazi tunawajibu wa kupinga vita kwa nguvu zote” alieleza Mbunge huyo.

Kwa upande wake katibu Uwenezi wa  Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mjini Maulid Issa alisema kwamba Serikali inatakiwa kulivalia njuga suala la udhalilishaji kwa kuweka adhabu kali kwa wafanyaji.

“Vitendo hivi vinazidi kukithiri kutokana na Serikali imeweka adhabu ambayo si kubwa ndo maana vinazidi kila kukicha, laity waweke mtu akikutikana na hatia basi anawekwa ndani miaka midogo 20 basi hakuna atakae fanya vitendo hivi” alisema Katibu huyo wa Unezi.

Kwa Mujibu wa Taarifa za Jeshi la Polisi Jumla ya matukio 826 ya udhalilishaji yameripotiwa kwa kipindi cha januari hadi Dicemba 2019 huku mwaka 2018 yakiripotiwa matukio 787.