Meya Dar apewa siku 14 kukabidhi ofisi, Mwenyewe ataka gari lake

Sakata la Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita limeendelea kuchukua sura mpya na sasa mkurugenzi wa jiji hilo, Sipora Liana amempa siku 14 akabidhi ofisi.

Wakati Sipora akimuandikia barua Mwita na kumpa siku 14 kuanzia Januari 10 kukabidhi ofisi, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema sintofahamu imegubika mchakato mzima wa kuvuliwa umeya Mwita hasa ikizingatiwa kanuni inavyoeleza sivyo ilivyotumika.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji kifungu cha 84 (1) kinaeleza ili uamuzi uweze kufanyika wa kumwondoa meya madarakani kutokana na sababu kadhaa, itapaswa kuwapo kwa theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri hiyo.

Theluthi mbili ya wajumbe 26 wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ni 17. Kifungu hicho kinasomeka:

“Halmashauri inaweza kumuondoa meya madarakani kwa kupata azimio linaloungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri kutokana na hoja au sababu yoyote zifuatazo mojawapo ni kutumia vibaya ofisi yake.”

Kikao maalumu cha baraza la madiwani la jiji hilo, Alhamisi iliyopita kilikutana kwa ajenda moja ya kupokea ripoti ya tuhuma dhidi ya Meya Mwita kisha kupiga kura ya kutokuwa na imani naye huku kura zilizomkataa zikiwa 16 pungufu ya matakwa ya kanuni za Halmashauri zinavyoelezwa.

Juzi, mkurugenzi wa jiji hilo, Sipora alilieleza Mwananchi kuwa tayari amemwandikia barua Meya ya kukabidhi ofisi.

Hata hivyo, Mwita ambaye ni diwani wa Vijibweni (Chadema) jana alisema amepokea barua hiyo ikimtaka akabidhi mali za ofisi hiyo ndani ya siku 14, lakini amesisitiza bado yeye ni meya wa jiji hilo.

“Ninatafakari na nitamwelekeza mwanasheria wangu amjibu mkurugenzi kuwa aheshimu taratibu na atambue kuwa mimi bado ni meya wa jiji hili. Ofisi ya mkurugenzi kuna wanasheria awatumie ili asivuruge mambo na Jumatatu nahitaji kuletewa gari ofsini,” alisema Mwita.

Kutokana na hilo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus alisema katika mchakato huo kuna dalili ya siasa imetumika badala ya kanuni kwa sababu kuu mbili mojawapo ni kanuni ya akidi kuwa na utata kidogo.

“Kama wajumbe waliotakiwa kuwepo kwenye halmashauri ndiyo waliotakiwa kufanya uamuzi kitendo cha kuwa na jina na sahihi ya mtu ambaye hajafika ni kukiuka kanuni na mchakato haukwenda kwa usahihi.

“Kosa la pili ni kuwa mchakato wa kumuondoa meya ulipaswa ushirikishe ofisi ya mkuu wa mkoa. Na siku ile alipaswa awepo mkuu wa mkoa au mwakilishi wake wa kuja kusoma tuhuma dhidi ya meya na ripoti ya uchunguzi na kuwauliza wajumbe kama wameipokea. Hilo halikufanyika,” alisema Kristomus.

Kwa mujibu wa Kristomus, hayo ndiyo makosa makubwa mawili yaliyofanyika katika mchakato huo na kwamba ilitakiwa Mkuu wa Mkoa Paul Makonda na kamati yake kuthibitisha kama meya ana makosa kwa mujibu wa uchunguzi wao.

Siku ya uwasilishaji wa ripoti hiyo, Makonda hakuwepo na mwanasheria wa jiji ndiye aliyeisoma.

“Sasa naona siasa za kujiandaa na uchaguzi wa mwaka huu zimeanza kwa kuanza kuwaonyesha wananchi kuwa Chadema haina uhalali wa kuongoza Dar es Salaam. Endapo Mwita akifanikiwa kuvuka kiunzi hiki bado atakuwa na wakati mgumu kufanya kazi na naibu wake na mkurugenzi wa jiji,” alisema.

Kristomus alisema kuna watu wawili wa kuokoa sintofahamu hiyo akisema wa kwanza ni Makonda anayetakiwa kujitokeza kueleza mwenendo wa mchakato mzima na kuhusu azimio la kumuondoa Mwita.

Alisema mtu wa pili ni waziri wa Nchi, Ofisi Rais (Tamisemi), Seleman Jafo ambaye anatakiwa kumwelekeza mkurugenzi au mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuanzisha upya mchakato, lakini busara ingeweza kutumika kama njia ya tatu.

“Kwanza ni kupima uzito wa tuhuma na athari za kisiasa na zikionekana kiuhalisia hazina mashiko basi aachwe amalize muda wake na watu wajipange kwa siasa za baadaye mwaka huu. Waingie kwenye sanduku la kura mwa mikakati mipya,” alisema mhadhiri huyo huku jitihada za kumpata Waziri Jafo zikigonga mwamba jana.

Wakili wa Kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema kuna makosa yamefanyika kwa mujibu wa kanuni za kudumu za halmashauri ya jiji la Dar es Salaam katika suala nzima la mchakato wa kupiga kura za kumuondoa meya huyo.

Dk Kyauke alisema Mwita ana nafasi ya kukataa rufaa kwa waziri mwenye dhamana Jafo kuashiria kuwa hajaridhika na mwenendo mzima wa azimio la kutokuwa na imani na yeye.

“Afuate utaratibu uliopo aenda kwa Jafo ambaye ana wanasheria watakaofafanua jambo hili. Lakini akienda kwanza mahakamani sidhani kama atafanikiwa atapigwa tu,” alisema Dk Kyauke.