https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mtambo wa kuchenjua dhahabu mgodi wa Buzwagi wateketea kwa moto Kahama | Muungwana BLOG

Mtambo wa kuchenjua dhahabu mgodi wa Buzwagi wateketea kwa moto Kahama

Na Paschal Malulu-Kahama



Mtambo wa kuchenjua dhahabu katika mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama mkoani Shinyanga umeteketea kwa moto baada ya hitilafu ya umeme kujitokeza wakati unawashwa kwa ajili ya kuanza kwa shughuli yake katika mgodi huo.

Taarifa za awali zinadai kuwa mtambo huo baada ya kuwashwa katika chumba cha kuwashia ulitoa moshi ambao sio hali yake ya kawaida iliyozoeleka na kupelekea wataalam wanaohusika na kuuwasha kulazimika kuuzima kwa muda ili kuona kinachoendelea ndio moto ulipolipuka na kuanza kuwaka.

Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama Inspector Duma Mohamed amesema walipokea taarifa ya ajali hiyo katika mgodi huo ili kwenda kuuzima walipofika wamebaini kuwa mtambo huo unatumika kuchenjua dhahabu unatumia mafuta ya Diesel na Petrol hivyo umeharibiwa kwa kiasi kikubwa.

Amesema licha ya kufanikiwa kuuzima moto huo ambapo mtambo huo hauwezi kufanya kazi tena hadi kuwekwa mwingine kwa sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo chake ikiwa mara kwa mara umekuwa ukifanyakazi bila hitilafu yoyote.

Duma amesema amewataka viongozi wa mgodi wa Buzwagi kuzingatia ushauri wa jeshi hilo ili kujiepusha na ajali za moto pamoja na kufanya ukaguzi wa mitambo yao kabla ya kuanza kw shughuli zao.

Aidha ajali hiyo ya moto imetokea majira ya saa tano asubuhi katika mgodi huo wa Buzwagi Gold mine ambapo jeshi la zimamoto wilayani Kahama limewataka viongozi wa mgodi huo kuzingatia maelekezo ya jeshi hilo juu ya vifaa vya kuzimia moto na ishara ya ajali pindi inapotaka kutokea.