Urusi: Nyaraka za mkutano wa amani wa Libya ziko tayari

Kaimu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema karibu nyaraka zote kwa ajili ya mkutano wa amani wa Libya ziko tayari, lakini mahasimu wa taifa hilo lililoharibiwa kwa vita wamekataa kuzungumza.

Madola makuu ya dunia yanajianda kufanya mkutano wa amani mjini Berlin Jumapili hii kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Lavrov amewaambia waandishi habari kuwa nyaraka za mwisho zinaonekana kuwa tayari, lakini akasisitiza juu ya mzozo mkubwa kati ya pande hasimu - ule wa mbabe wa kivita Khalifa Haftar wenye makao yake mashariki mwa nchi, na serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mapema wiki hii, viongozi hao wawili walihudhuria mazugumzo mjini Moscow lakini Haftar aliondoka ghafla siku ya Jumanne bila kusaini mapatano ya kudumu ya kumaliza mapigano yaliyodumu kwa miezi tisa sasa.