Wanahabari wametakiwa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF)



Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Wanahabari nchini wametakiwa kujiunga na Mfuko wa Taifa  wa Bima ya Afya  (NHIF)  ili waweze kupata matibabu ya uhakika pindi wanapopata magonjwa  na  kutokuathiri  majukumu yao ya kuhabarisha umma bila vikwazo vya kiafya .

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa  wa Bima ya Afya ( NHIF) ,Christopher Mapunda wakati akizungumza katika kikao kazi cha mfuko huo na Wanahabari chenye lengo la kukuza uelewa wa wanahabari juu ya mfuko huo ili waweze kuhabarisha umma juu ya manufaa ya mfuko huo.


Mapunda amesema kuwa mfuko huo umelenga kumfikia kila Mtanzania ikiwa ni pamoja na kushirikisha sekta zisizo rasmi ikiwemo Wanahabari,Bodaboda na Mama Ntilie ambao wanavifurushi vyao maalumu vinavyowawezesha kuchangia na kupata uhakika wa huduma za afya.

“Tuondokane na kasumba za kusubiri mtu akiumwa achangiwe tupitishe bakuli bali watu wajiunge na bima yetu ya NHIF ili wachangie kabla ya kuugua na watakapopatwa na magonjwa wanapata matibabu  mazuri kupitia huduma zetu” Anaeleza Kaimu Mkurugenzi.

Meneja wa NHIF mkoa wa Arusha,Isaya Hendry  amesema kuwa ataendelea kushirikiana na wanahabari katika kutoa taarifa za fursa za mfuko huo kwa wananchi kupitia vifurushi mbalimbali vya Najali Afya,Wekeza Afya na Timiza Afya.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC) ,Claud Gwandu amewataka Wanahabari kujiunga  kwa wingi katika Mfuko wa taifa wa bima ya afya ili kutunza afya zao na familia zao hata wanapopata magonjwa inakua rahisi kupata matibabu ya uhakika.