Waziri Mhagama azitaka PSSSF, NSSF kufungua vituo vidogo kusaidia wazee na wastaafu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama ameutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kufungua vituo vidogo katika Wilaya zote nchini ili kuondoa usumbufu kwa wastaafu na wazee wasiojiweza kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufanya uhakiki wa taarifa zao.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo Jumatano, Januari 15, 2020 Mkoani Manyara wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa majukumu ya sekta ya hifadhi ya jamii Mkoani humo, na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haipo tayari kuona wastaafu na wazee wakipata usumbufu kwa ajili ya malipo ya pensheni zao.

Aliongeza kuwa Serikali inatambua kuwa uhakiki ni zoezi endelevu na wastaafu na wazee wanapaswa kutii agizo hilo, hivyo ni wajibu kwa mameneja wa Mikoa wa mifuko ya NSSF na PSSSF kuhakikisha wanaweka utaratibu mwepesi na rafiki kwa wastaafu hao kwani wapo ambao hawawezi kutembea umbali mrefu kutokana na changamoto mbalimbali.

‘Mnapokwenda kuwahakiki wagonjwa, nawaomba pia mfungue vituo vya kuwahakiki watu wazee na watu wazima sana, wahakikiwa waende kukutana nanyi maeneo ya wilayani, hivyo nawaomba mtengeneze ratiba na kuweka utaratibu mwepesi na rafiki kwa wastaafu, na agizo hili ni kwa nchi nzima si hapa Manyara pekee’’.

Waziri Mhagama alitolea mfano kwa Mkoa wa Manyara ambao wazee na wastaafu wengi wamekuwa wakitembea umbali kwa ajili ya kufika Makao makuu ya mifumo hiyo iliyopo Mkoani, suala ambalo limekuwa likiwaumiza wazee na wastaafu wengi hususani wale wasio na watoto au wasaidizi wa kuwafikisha katika Ofisi hizo.

Aidha Waziri Mhagama alisema kufunguliwa kwa vituo hivyo kutasaidia kuokoa muda wa kufanya uhakiki na taarifa za wastaafu na wazee wote kupatikana kwa haraka na kuwasilishwa mapema katika Makao makuu ya mikoa na hivyo kuharakisha upatikanaji wa mafao ya wastaafu hao kwa wakati.

Akifafanua zaidi Waziri Mhagama alisema Serikali inatambua kuwa zoezi la uhakiki wa wastaafu na wazee katika mifuko hiyo bado linaendelea katika maeneo yote nchini, hata hivyo Serikali imeendelea kusisitiza kwa mifuko hiyo kuongeza kasi katika malipo ya pensheni na mafao ya wastaafu na wazee hao kwa wakati.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama alisema Serikali inaendelea kusisitiza mamlaka zote zinazohusika nchini kuhakikisha zinashirikiana ili kuweza kubaini changamoto zinazojitokeza wakati wa mchakato wa malipo mafao ya wastaafu na wazee wote nchini ili kuweza matatizo ya kimfumo na kiutendaji yaliyopo katika maeneo yao.

Waziri Mhagama aliitaka mifuko hiyo kuendelea kuchukua hatua kwa Ofisi zote za Serikali na binafsi zinazodaiwa michango ya wanachama ipo pale pale na hakuna msamaha unaoweza kutolewa, na kuwasilisha taarifa kwa ofisi zote zinazotaka kuwa wadaiwa sugu ili kuweza kuzichkulia hatua stahiki.

‘Kama ndani ya halmashauri kuna kuna matatizo ya kimfumo na kiutendaji, ni wajibu wetu kutoa taarifa katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu Wilaya na wao watasaidia kuwasiliana na Wizara husika kutatua matatizo hayo yanayojitokeza ambayo yanaweza kuchelewesha mafao ya wanachama, taarifa hizi hazina budi kuwasilishwa haraka iwezekanavyo’’.

Aliongeza kuwa kwa sasa Serikali ipo katika mchakato wa kipindi cha mpito katika utekelezaji maagizo ya Rais Dkt. John Magafuli, ambapo Ofisi yake imejipanga kuhakikisha kuwa Mifuko ya hifadhi ya jamii inatoa mafao yanayoendana na hali halisi ya nchi pamoja na kuzingatia wakati na viwango endelevu.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Matekelezo na Mafao wa (NSSF) Adolfrida Mulokozi alisema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba mfuko huo tayari umelipa kiasi cha Tsh. Bilioni 1.036 pamoja na kushughulikia madai 26 ya pensheni za wazee.

Aidha alisema kwa upande wa usajili, Mfuko huo kwa Mkoa wa Manyara umeweza kusajili wanachama 1926 wakiwemo wanachama 1062 kutoka katika sekta rasmi na wanachama 864 wa sekta isiyo rasmi.