Zaidi ya Bilioni 8.5 zatumika kukarabati na kujenga kituo kipya Cha kufua Umeme, ATC.


Na Ezekiel Mtonyole

Zaidi ya shilingi bilioni 8.5 zimetumika kukarabati na kujenga  majengo mpya ya kituo cha mafunzo ya kufua umeme kwa kutumia nguvu  za maji cha Kikuletwa kinachomilikiwa na Chuo cha Ufundi Arusha , ATC.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa  kituo hicho Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema uendelezaji wa kituo hicho ni sehemu ya mpango mkakati wa Serikali wa uboreshaji utoaji wa Elimu ya Ufundi nchini kwa kutoa mafunzo kwa vitendo.

Amesema  mfumo huo utawezesha kupata wahitimu walio mafundi mahiri waliobobea katika fani ya kufua umeme.

“Elimu itakayopatikana hapa itawasaidia vijana kuitumia elimu hiyo kujiajira kwani kuna fursa nyingi kwenye kujiajiri kuliko kusubiri fursa chache zilizopo za kuajiriwa, nina uhakika vijana wanaotoka hapa watakuwa mahiri katika kufua umeme ” amesema Ole Nasha

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa uanzishaji wa Kituo cha mafunzo cha kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji hapa Kikuletwa umelenga kuongeza watalaamu; hasa mafundi stadi (artisans) na mafundi sanifu (technicians) ambao atashiriki katika ufuaji wa umeme kutoka vyanzo vidogo vidogo vya maji na vikubwa pamoja kufanya tafiti juu ya nishati jadidifu (Research in renewable energy) ikiwemo uzalishaji umeme kutokana na nguvu ya maji.

Ole Nasha amesema serikali inatambua umuhimu wa Elimu ya ufundi kuelekea Tanzania ya viwanda ambapo inaendelea kufanya uwekezaji mkuwa katika vyuo vya ufundi, uwekezaji ambao umeongeza udahili na ubora katika Elimu ya ufundi.


Kutokana na uwekezaji unaoendelea idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi imeongezeka kutoka 30,000 mwaka 2015 hadi 151,969 mwaka 2019 pia inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi 43 kwa gharama ya shilingi bilioni 92 katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na ujenzi wa chuo kipya Jijini Dodoma chenye hadhi sawa na ATC au DIT kwa gharama ya shilingi bilioni 18.

Aidha, Naibu Waziri ameongeza kuwa serikali imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa Elimu ya Ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 75 unaolenga kuleta mapinduzi katika Elimu ya ufundi nchini kwa kuvijengea vyuo uwezo ili viweze kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi stahiki, ujenzi wa miundombinu bora, kuweka vifaa na kuwajengea uwezo wakufunzi.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Dkt.Masudi Senzia amesema kuwa tayari kituo hicho kimeanza kupokea wanafunzi ambao wanapata mafunzo katika fani mbalimbali za kufua umeme ambapo vijana wanaouzunguka eneo la Kikuletwa wamejitokeza kwa wingi​ kwa ajili ya kupata elimu itayowaezesha kujikwamua kimaisha.

Masudi ameongeza kuwa kupitia ufadhili wa benki ya dunia kituo kitaendelea kupanuliwa ili kiweze kuhudumia nchi za Afrika Mashariki kama kituo cha umahiri .

Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania Elizabeth Jacobsen amesema kuwa Norway itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania kwa kuendelea kusaidia  na kuijengea uwezo Vyuo katika masuala ya nishati jadidifu itakayosaidia kufikia uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda.

Balozi Elizabeth amesema kuwa kituo hicho kitasaidia katika mafunzo ya jinsi ya kuongeza uzalishaji wa umeme unaotokana na maji katika maeneo mbalimbali nchini huku ukilenga kujenga wataalamu waliobobea katika kufua umeme.

Mkuu wa Wilaya ya Hai,Lengai ​ Ole Sabaya amewataka wananchi kushirikiana na kituo hicho katika kulinda miundombinu iliyoko ili iweze kuwanufaisha vyema watu wa Hai,Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.