Faida ya binzari kiafya

Binzari ni kiungo ambacho hutumiwa sana jikoni kwa ajili ya kusaidia kubadili rangi ya vyakula, lakini si wengi wanaofahamu kwamba kiungo hiki kinamanufaa kiafya pia hasa pale kinapotumika vizuri.

Lakini kabla ya kuanza kueleza faida hizo za binzari ni vyema tuambizane kuhusu hii binzari maana huenda wengine hawaifahamu vizuri. Binzari muonekano wake inataka kuendana na tangawizi kwa mbali na pale inaposagwa basi huwa tunapata unga wake ambao unatambulika zaidi kama 'manjano'

Kwanza kabisa matumizi ya binzari husaidia sana kumkinga mhusika dhidi ya magonjwa ya saratani hususani saratani ya tezi dume, lakini pia binzari inauwezo mzuri wa kupambana na seli ambazo huweza kuchochea mtu kupatwa na saratani.

Aidha, matumizi ya binzari husaidia sana kwa wale wenye shida ya kukumbwa na maumivu kwenye maungio ya mifupa 'Arthritis' .

Binzari pia inauwezo mzuri wa kushusha sukari ndani ya mwili hivyo huwafaa wale wenye tatizo la ugonjwa wa sukari hususani diabetes type 2, lakini pia kiungo hiki husaidia sana kupambana na mrundikano wa mafuta hatari ndani ya mishipa ya damu 'Cholesterol'.

Mhusika anapotumia kiungo hiki cha binzari husaidia kupunguza 'Cholesterol'. ndani ya mishipa ya damu na hivyo kumuepusha mhusika dhidi ya matatizo ya moyo.

Kazi nyingine ya binzari ni kusaidia kuimarisha kinga za mwili hii ni kwa sababu ndani ya kiungo hicho kuna kirutubisho kiitwacho 'lipopolysaccharide,' ambayo husaidia kuamsha kinga za mwili na kuzifanya kuwa imara zaidi.

Lakini pia binzari ni moja ya kinga nzuri ya bakteria, fungusi, na ikiwa utakuwa unahisi homa unaweza kupata kijiko kimoja cha unga wa binzari na kuchanganya na maziwa ya moto kiasi glasi moja kisha kunywa kwamara moja.