Hong Kong kutoa ruzuku huku kirusi cha Corona kikichangia kudorora kwa uchumi

Hong Kong leo imetangaza ruzuku ya fedha kuzisaidia biashara ambazo zimeathirika kutokana na kuzuka kwa kirusi cha Corona katika mji ambao tayari unakumbwa na kushuka kwa uchumi.

Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China pamoja na miezi kadhaa ya maandamano ya kupigania demokrasia mwaka jana, tayari vilikuwa vimeusukuma uchumi wa eneo hilo la kibiashara katika viwango vya chini.

Kirusi hicho kimeongezea katika masaibu hayo na kupeleka kupungua kwa idadi ya watalii wanaowasili katika eneo hilo huku biashara ndogo zikifilisika. Hii leo, kiongozi wa jimbo hilo, Carrie Lam, amesema kuwa serikali itatumia hifadhi yake ya fedha kutoa ruzuku kwa sekta zilizoathirika zaidi kutokana na mzozo huo.