Mahakama ya Uingereza yaamuru kwamba ndoa za Kiislamu ni haramu

Mahakama moja imebadilisha uamuzi wa miaka miwili iliopita kwamba wanandoa waliooana kupitia sheria ya Kiislamu wana haki ya kutalakiana.

Mahakama kuu iliamuru 2018 kwamba wanandoa hao waliofanya ndoa ya Kiislamu ya 'nikah' walioana kulingana na sheria ya ndoa ya Uingereza.

Lakini mahakama ya rufaa sasa imesema kwamba ndoa hiyo ilifanyika kinyume na sheria na hivyobasi ni haramu.

Majaji walisema kwamba kwa kuwa walitaka kufanya sherehe nyengine ya kiraia - ilimaanisha kwamba walifahamu kuwa ndoa yao iliofanyika kwa mujibu wa sheria za Kiislamu ilikuwa kinyume na sheria za Uingereza.

Mwanasheria mkuu alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa kwanza wa mahakama.

Kesi hiyo ilihusu kutalakiana kwa Nasereen Akhter na Mohammed Shabaz ambao wana watoto wanne.

Wanandoa hao walifanya sherehe ya Kiislamu katiika mkahawa mmoja wa kaskazini mwa London 1988 mbele ya Imamu na takriban wageni 150, lakini hakuna sherehe ya kiraia iliofanyika licha ya bi Akhter kuwasilisha ombi hilo.

Walitalakiana 2016 na bwana Khan alijaribu kuzuia ombi la mkewe la kutalakiana miaka miwili iliopita kwa misingi kwamba hawakuoana kisheria,

Bi Akhter alihoji kwamba ndoa yao iliofanyika Kiislamu ilikuwa halali mbali na ombi lake la kutalakiana na kwamba alihitaji kulindwa kisheria na kwamba kesi hiyo ilihitaji kutatuliwa kisheria kama wanandoa wengine nchini Uingereza.

Ombi lake la kutaka talaka lilijadiliwa wakati alipoliwasilisha katika kitengo cha familia katika mahakama hiyo na jaji Williams aliandika uamuzi wake mwisho wa msimu wa 2018.

Aliamuru kwamba kwa kuwa wanandoa hao walijionyesha kwa umma kama mke na mumewe, bi Akhter alikuwa sawa na kwamba ndoa yao inafaa kutambuliwa kwa kuwa kiapo walichokula katika dini ya Kiislamu kina malengo sawa na kile cha wanandoa wa Uingereza.

Aliongezea kwamba ndoa hiyo iliafikia sheria ya 1973 ya ndoa, licha ya bwana Khan kuhoji kwamba ndoa hiyo ilifanyika chini ya sheria ya Kiislamu pekee.

Jaji Williams alisema kwamba bi Akhter alikuwa na haki ya amri ya ubatili wa ndoa hiyo.

Lakini mahakama ya rufaa ilibatilisha uamuzi huo siku ya Ijumaa na kusema kwamba ndoa hiyo ilikuwa haramu chini ya sheria za ndoa za Uingereza.

Ilielezea kwamba ndoa hiyo sio sheria iliofuzu kwa sababu haikufanyika katika jumba lililosajiliwa kuandaa harusi, hakuna vyeti vilivyotolewa na hakuna msajili wa ndoa aliyekuwepo.

''Wawili hao hawakuooana chini ya sheria za Uingereza'', alisema jaji wa mahakama ya rufaa.

Kati ya wanandoa hao wawili hakuna mmoja wao aliyeshiriki katika rufaa hiyo.

Pragna Patel Mkurugenzi wa shirika la Southall Black Sisters alisema: Uamuzi wa leo utawalazimu Waislamu na wanawake wengine kwenda katika mahakama za Kiislamu ambazo zinawadhuru pakubwa wanawake na watoto katika kupata haki kwa kuwa sasa wamezuiwa katika mfumo wa raia wa kupata haki.

Hatua ya serikali ya kuangazia upya sheria ya Kiislamu 2017 ilisema kwamba wanandoa Waislamu watahitajika kushiriki katika ndoa za kiraia mbali na sherehe za Kiislamu ili kuweza kuhalalisha ndoa za Kiislamu sawa na zile za Kikristo pamoja na zile za Kiyahudi.