Mbunge wa Babati Vijijini asisitiza Wananchi wakitumie Chuo Cha VETA Manyara



Na John Walter-Babati

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Vrajlal Jituson (CCM) amewataka wananchi wa jimbo lake waliokumbwa na Mafuriko na miundo mbinu ya bara bara kuharibiwa,  wawe watulivu kwani serikali imeshaanza kuchukua hatua na muda wowote Wakala wa Bara bara vijijini Mijini (TARURA) na Wakala wa Bara bara mkoa wa Manyara (TANROADS) ,watafika katika maeneo hayo yaliyoathiriwa na kuyarejesha katika hali  ya kawaida.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Jituson alitoa hamasa kwa wananchi wa jimbo la Babati vijijini  katika maeneo ambayo tayari miundombinu ya umeme imefika, kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe huduma hiyo.


Mbunge huyo ameeleza hayo alipokutana na wananchi wa kijiji cha Ufana kata ya Ufana kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili ili zitafutiwe ufumbuzi.

Mpaka sasa Vijiji zaidi ya 140 wilayani Babati vimenufaika na mradi wa  umeme vijijini  (Rea)  ujenzi wa zahanati mpya 18 na vituo vya afya tisa.

Aidha amesema kuwa jimbo hilo amelifanyia mambo mengi katika Nyanja mbalimbali  ikiwa ni pamoja na Afya pamoja na Elimu ambapo kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wameweza kujenga tawi la Chuo hicho katika eneo la kata ya Ayasanda yenye vijiji viwili vya  Endanachan na Ayasanda ambacho kitawawezesha waliohitimu darasa la saba,kidato cha nne na sita kujifunza fani mbalimbali.

Amewataka wananchi wa Babati kutumia vizuri chuo hicho kuwapeleka watoto wao wakapate elimu.

Mkutano huo umekuja baada ya wazee kumuomba diwani wa kata hiyo kumuita  Mbunge huyo ili azichukue kero hizo na kuzifikisha kwa wahusika.