Mkuu wa wilaya ya Mbinga awataka madereva waheshimu sheria za barabarani



Na Ahmad Mmow, Mbinga.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, mkoa wa Ruvuma, Cosmas Ishenye amewataka madereva wa vyombo vya moto wilayani humo waheshimu sheria za barabarani ili kuepuka ajali za mara kwa mara , hasa mjini Mbinga.

Ishenye ambae ni mwenyekiti wà kamati ya ulinzi ya wilaya ya Mbinga alitoa agizo kwenye mazishi ya  mwenyekiti wà baraza la wazee wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) wilaya ya Mbinga na msaaidizi wa kisheria wa kituo cha Nafuu ya Jamii Tanzania( NAJATA), Samuel Kayuni aliyefariki juzi kwa ajali ya barabarani.

Alisema nijambo lakusikitisha na lisilokubalika kuona ajali za mara kwa mara zinazosababishwa na madereva wasio heshimu na kutii sheria bila shuruti. Kwahiyo madereva hawanabudi kuheshimu sheria.

Katika kuhakikisha agizo lake linafanyiwa kazi kikamilifu, amemtaka kamanda wa polisi wa wilaya( OCD) kupitia kitengo cha usalama barabarani kufuatilia kwa karibu mienendo ya madereva ili kuwachukulia hatua sitahiki za kisheria wasio heshimu na kutii sheria.

" Kila mara nasikia ajali za barabarani, sijui zinatokana na uzembe au kutojua sheria? Sasa OCD fuatilia ili muwachukulie hatua wanaovunja sheria na kusababisha ajali," Ishenye alihoji na kuagiza.

Mbali na maagizo hayo kwa madereva na jeshi la polisi wilayani humu, mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga aliwaasa watembea kwa miguu na hata waendesha baiskeli wazingatie usalama wao kwa kuheshimu na kutumia vema alama za usalama barabarani.