Mwongozo kwa wanafunzi wa kigeni nchini China watolewa

Serikali ya China imetoa mwongozo kwa wanafunzi wa kigeni wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu nchini humo, wakiwemo wa Tanzania wakati jitihada za kupambana na virusi vya Corona zikiendelea.

Mwongozo huo umewataka wanafunzi hao kutorejea vyuoni hadi  watakapopewa taarifa rasmi kutoka mamlaka za vyuo vyao.

Pia, wametakiwa kufanya mawasiliano na vyuo vyao ili kupata taarifa kama kozi zao zitaendeshwa kwa njia ya mtandao na muda wa kuanza masomo hayo.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Tanzania nchini China imewataka wanafunzi wa kigeni kuzingatia na kufuata masharti, maelekezo na miongozo inayotolewa kwa ajili ya afya zao na ustawi kwa ujumla.                     

Maelekezo hayo yametolewa pia kwa wanafunzi wote wa kigeni ambao vibali vyao vya kuishi au Visa vinakaribia kumalizika muda wake, wametakiwa kufika katika ofisi za uhamiaji kuongeza muda wa kupata nyaraka hizo mpya haraka.

Kulingana na taarifa ya serikali ya China katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya Corona, ofisi za uhamiaji zitakuwa wazi kutoa huduma, hivyo raia wa kigeni watumie nafasi hiyo kupata huduma hizo.