Rais Hassan Rouhani asema Trump hataki vita na Iran

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema haamini kama Marekani itaingia katika vita na Jamhuri hiyo ya Kiislamu, kwa sababu jambo hilo litaiharibu azma ya Rais Donald Trump kuchaguliwa kwa mara nyengine katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Kiongozi huyo wa Iran ameongeza pia kwamba vita vitakuwa na madhara kwa maslahi ya Marekani na marafiki zake wa kikanda pamoja na Iran.

Iran na Marekani zilikaribia kuingia kwenye vita mwezi Januari baada ya shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa Iran, Qasem Soleimani, nje ya mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Iran ilijibu kwa kurusha makombora katika kambi ya jeshi iliyokuwa na wanajeshi wa Marekani.

Mivutano imekuwa ikiongezeka kati ya Iran na Marekani tangu Rais Trump aiondoe Marekani kutoka kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 na kuiwekea Iran vikwazo kwa mara nyengine tena.