Rwanda: Polisi inasema msanii maarufu wa nyimbo za injili Kizito Mihigo amejinyonga

Polisi ya Rwanda imetangaza kwamba msanii maarufu wa nyimbo za injili,Kizito Mihigo ''amejinyonga'' Polisi wa Rwanda wanasema.

Kwa mjibu wa tangazo la polisi maiti ya msanii huyo imepatikana katika chumba alimokuwa anazuiliwa kwenye kituo cha polisi mtaa wa Remera,mjini Kigali.

Polisi imesema kwamba amejinyonga siku tatu baada ya kukamatwa karibu na mpaka baina ya Rwanda na Burundi katika kile ambacho polisi ilisema alikuwa na nia ya kutoroka nchi na kujiunga na makundi ya waasi dhidi ya Rwanda.

Alikuwa ameanza kufanyiwa uchunguzi kuhusu madai hayo pamoja na kutaka kuwahonga wananchi waliomkata.

Mwaka uliopita aliachiwa huru kwa msamaha wa rais baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa hatia ya kutaka kumuua rais na kuhamasisha raia kupinga serikali.