Serikali yasaini mikataba ujenzi wa barabara ya Kabingo


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), imesaini mikataba minne ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kabingo - Kasulu – Manyovu mkoani Kigoma, yenye urefu wa kilometa 260.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo mkoani humo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36 na utagharimuJumla ya shilingi bilioni 585.

"Leo tupo hapa tukiwa na furaha kubwa kushuhudia tukio hili muhimu na la kihistoria katika mkoa huu, kusainiwa kwa mikataba hii ni kutimia kwa ndoto na ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli ya kuifungua Kigoma kiuchumi na kijamii kwa kuiunganisha kitaifa na kimataifa kutokana na barabara hii kuunganisha nchi za jirani za Burundi, Rwanda na DRC - Congo", amesema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe ametaja makampuni yaliyopata zabuni ya kutekeleza mradi huo kuwa ni Zhejing Communication Construction Group Company Ltd (ZCCC), Sinohydro Corporation Ltd, Stecol Corporation na China Henan International Corporation (CHICO) ambapo utekelezaji wa mradi huo umegawanywa sehemu nne.

“Kama ambavyo mmemsikia Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuwa mradi huu utatekelezwa na makandarasi hawa kwa sehemu nne, sehemu ya kwanza itahusisha ujenzi wa barabara kuanzia Kasulu junction – Manyovu na viunganishi vya barabara za Kasulu mjini (Km 68.25), sehemu ya pili itakuwa ni Kanyani- Kidyama- Mvugwe (Km 70.5), ya tatu ni Mvugwe- Njia panda ya Nduta (Km 59.35) na ya mwisho ni Nduta junction – Kabingo junction (Km 62.5),” amefafanua Mhandisi Kamwelwe.

Aidha, Mhandisi Kamwelwe amewataka makandarasi waliopata zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha wanatekeleza ujenzi wake kwa mujibu wa mikataba na kuwasisitiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanawasimimia makandarasi hao ili kupata barabara yenye kiwango sawa na thamani ya fedha iliyotumika.

Waziri Kamwelwe, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuboresha miundombunu ya barabara katika uwanda wa magharibi ili kuifungua Kigoma na mikoa mingine ya jirani.

“Serikali hii hailali inafanya kazi usiku na mchana, miradi ya ujenzi wa barabara kama ya Chaya - Nyahua (km 85.4), Chagu- Kazilambwa (km 36) na Kaliua - Urambo (km 28) inaendelea kujengwa na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu”, amebainisha Kamwelwe.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kati ya Mkoa huo na mikoa ya jirani pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi na DRC- Congo

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaenda sambamba na uboreshwaji wa huduma za afya pamoja na elimu kwa kujenga shule, zahanati pamoja na ununuzi wa magari manne ya wagonjwa ambazo zitasaidia katika kuleta maendeleo mkoani humo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga, amesema kuwa ujio wa mradi huo mkoani kwake utapelekea uzalishaji wa ajira kwa vijana na kuimarika kwa huduma za usafiri na usafirishaji.