Sumaye: CCM ni nyumbani, nipo tangu TANU


Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye ametangaza kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni takribani miaka mitano tangu alipoondoka.

Sumaye ametangaza uamuzi huo jijini Dar es salaam  na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally.

"Naomba mnipokee nimerudi nyumbani, nimekaa CCM tangu TANU na baadae nikawa kati ya Wanachama waanzilishi wa CCM nikashika nafasi nyingi za uongozi na kuingia Bungeni 1985 hadi 2005, nimeshakuwa Naibu Waziri baadae Waziri kisha Waziri Mkuu nikiwa CCM, CCM ni nyumbani” alisema Sumaye.

Agosti 22 mwaka 2015 Sumaye alijitoa CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikiwa ni moja ya vyama vilivyokuwa vikiunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Baada ya kukitumikia chama hicho kwa zaidi ya miaka minne, Disemba 4 mwaka 2019 alitangaza kujitoa CHADEMA kwa kile alichosema kwamba alidhani ndani ya chama hicho kungekuwa na demokrasia lakini haikuwa hivyo.

Licha ya kujitoa CHADEMA alisema hajiungi na chama chochote cha siasa na kwamba angebaki huru na kuendelea kutoa ushauri kwa chama chochote ambacho kingemhitaji wakati wowote.

Miezi miwili baada ya kutoa kauli hiyo amejiunga CCM, akiwa ni kiongozi wa pili wa ngazi ya juu kurudi CCM baada ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowasa kurudi CCM mwezi Machi mwaka 2019 akitokea CHADEMA, chama alichojiunga nacho mwezi Julai mwaka 2015.