Wakili wa Kijitegemea Abdul Lyana afikishwa mahakamani kesi ya uhujumu uchumi


Wakili wa Kijitegemea Abdul Lyana anayeishi Mbezi Makonde jijini Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la kuratibu genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha na kutakatisha zaidi ya USD 26,250 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh. Milioni 60.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali  Glory Mwenda amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mbando kuwa kati ya Januari Mosi na Desemba 30 mwaka jana  jijini Dar es Salaam mshtakiwa akiwa na wenzake ambao bado hawajakamatwa waliongoza genge la uhalifu kinyume na sheria kwa lengo la kujipatia fedha.

 Katika shitaka la utakatishaji fedha imedaiwa siku na mahali hapo mshtakiwa Lyana na wenzake  hao kwa njia ya udanganyifu walijipatia zaidi ya Sh. Milioni 60 kutoka kwa Yasser Abdelhamad  kwa kujifanya kuwa wangemuuzia tani 25 za madini ya shaba.

Hata hivyo mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Pia upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili kutajwa.