Yanga kuzisaka point tatu za Tanzania Prisons

UONGOZI wa Yanga umesema kuwa mchezo wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons hautakuwa mwepesi kutokana na ugumu wa timu ambayo watakutana nayo.

Prisons itashuka Uwanja wa Taifa kumenyana na Yanga, Februari 15, majira ya saa 1:00 usiku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi zote mbili msimu huu ilipokutana na Yanga.

Mechi ya kwanza ya ligi ilichezwa Uwanja wa Samora na Prisons ilifungwa bao 1-0 lilifungwa na Patrick Sibomana na mechi ya pili ya Kombe la Shirikisho ilipigwa Uwanja wa Taifa ilikubali kichapo cha mabao 2-0 yaliyofungwa na Ikpe pamoja na Morrison.

Luc Eymael, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa wanatambua uimara wa wapinzani wao jambo litakalofanya mchezo kuwa mgumu.

"Haitakuwa kazi rahisi na mchezo utakuwa mgumu ila kikubwa ni maandalizi ambayo tunayafanya na mpaka sasa tupo vizuri, mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti," amesema.

Yanga ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 38, Prisons ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 25.